Tusibweteke na kilichotokea Sweden, hali bado ni tete Yemen- Lowcock

14 Disemba 2018

Matumaini kuhusu mustakabali wa Yemen kufuatia matokeo ya mkutano kati ya pande kinzani huko Sweden, yasisababishe tubweteke kwa kuwa bado hayajawa na athari ya moja kwa moja kwa wananchi wa kawaida.

Hiyo ni sehemu ya hotuba ya mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa dharura, OCHA, Mark Lowcock, wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo, kikao ambacho kimehutubiwa kwa njia ya video na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Martin Griffiths kutoka Amman, Jordan.

Bwana Lowcock amesema kuwa hakuna sababu ya kubweteka kwa kuwa ziara yake ya wiki mbili zilizopita nchini Yemen zimemkutanisha na madhila ambayo bado yanakumba mamilioni ya raia.

“Nimejionea mwenyewe, nimezungumza na familia ambazo zimekimbia mapigano kwenye jamii zao, baadhi  yao kwa miaka kadhaa sasa wanaishi kwenye nyumba zilizotengenezwa kwa makaratasi ya nailoni. Nimekutana na wazazi ambao kila wakati wanakimbilia hospitali kusaka tiba za watoto wao wenye utapiamlo,” amesema Lowcock akibainisha kuwa alichoona ni kile ambacho kila wakati kinaelezwa na mashirika ya kibinadamu ya kwamba ‘janga la kutisha linaibuka Yemen.’

Amesema na  hali inakuwa mbaya kwa hiyo, ‘habari njema kutoka Sweden wiki hii kama zilivyoelezwa na Bwana Griffiths kuhusu makubaliano kati ya serikali na wahouthi yasitufanye tufikirie kuwa sasa kila kitu ni shwari,” amesema Lowcock akiwajulisha wajumbe kuwa, “kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu tunaona dalili, pengine mambo yanaanza kuwa mazuri. Lakini raia niliokutana nao bado hawajashuhudia mabadiliko thabiti. Ahadi lazima zitekelezwe na harakati kuelekea amani lazima kasi iongezwe.”

Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA akihutubia Baraza la Usalama la UN hii leo Desemba 14, 2018
UN/Eskinder Debebe
Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA akihutubia Baraza la Usalama la UN hii leo Desemba 14, 2018

Bwana Lowcock ametumia kikao hicho kukumbushia wajumbe mambo matano ambayo aliwaomba mwezi Novemba kuwa watimize ambayo amesema hadi sasa hayajatimizwa ipasavyo ili kuleta nuru kwa wayemen.

Mambo hayo ni mosi, sitisho la mapigano akisema mapigano  yamepungua tu baadhi ya maeneo na pengine makubaliano kuhusu Hudaydah yanaweza kuleta sitisho la kweli. Pili ni kulinda usambazai wa vyakula na bidhaa muhmu akitaka kuondolewa kwa vikwazo vya safari katika baadhi ya maeneo ikiwemo bandari ya Hudaydah. Jambo la tatu ni utulivu wa kiuchumi akisema bado thamani ya sarafu ya Rial kwa dola ya Marekani ni chini hivyo ni lazima usaidizi zaidi hasa kwa bajeti ya Yemen kwa mwaka ujao ili kuongeza mzunguko wa fedha.

Suala la nne kwa mujibu wa Lowcock ni  kuongeza mchango kwenye ombi la Umoja wa Mataifa kwa usaidizi wa Yemen kwa kuwa mahitaji yataongezeka mwakani akigusia mkutano wa kuchangia Yemen ambao Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ataitishi huko Uswisi tarehe 26 mwezi Februari mwakani. Mkuu  huyo wa OCHA ametaja eneo la tano kuwa ni pande zote kuendelea kushiriki kwenye mchakato wa amani kwa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Sweden.

“Bwana Rais, maeneo  hayo matano ninayosisitiza ni kwa ajili  ya  kukumbusha kuwa ni kifurushi na si suala moja moja, tunataka  hatua katika vipengele vyote. Bila kujali kilichotokea Sweden, muhimu ni kwamba tuna safari ndefu,” ametamatisha Bwana Lowcock akisema wanachotaka wao ni msaada wa dhati kutoka Baraza la Usalama.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter