Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushikamane tutokomeze kauli za chuki- Guterres

Manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa ni mwaka 1998  wakati wakiwa kwenye eneo la Mwurire nchini humo ambako kulifanyika mauaji.
UN/Milton Grant
Manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa ni mwaka 1998 wakati wakiwa kwenye eneo la Mwurire nchini humo ambako kulifanyika mauaji.

Tushikamane tutokomeze kauli za chuki- Guterres

Amani na Usalama

Ikiwa leo ni miaka 25 tangu mauaji ya watutsi nchini Rwanda, Umoja wa Mataifa umepigia chepuo harakati za kuondokana na vitendo vinavyoweza kuchochea chuki.

 

Katika ujumbe wake wa siku hii ya leo ya kumbukizi ya mauaji hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema hata hivyo kumbukizi hiyo ya mauaji ya watutsi 800,000 na wahutu wa msimamo wa kati inafanyika, “bado tunashuhudia mielekeo hatari ya chuki dhidi ya wageni, ubaguzi na ukosefu wa stahamala maeneo mbalimbali duniani.”

Ametolea mfano jinsi ambavyo hivi sasa kuna kuli za chuki na uhamasishaji wa ghasia akisema, “ni kinyume na maadili yetu na zinatishia haki za binadamu, utulivu wa kijamii na amani.”

Bwana Guterres amesema pindi vitendo hivyo vinatokea, lazima vikabiliwe na vizuiwe kama ambavyo ilikuwa kwa uhalifu wa chuki na mauaji ya halaiki.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, kiduni na kiraia wapinge kauli za chuki, ubaguzi na wafanye kazi kwa dhati kushighulikia na kupunguza vyanzo vya vitendo hivyo ambavyo amesema vinaharibu utengamano wa kijamii.
 
“Uwezo wa vitendo vibaya upo kwenye jamii yetu lakini vile vile kama ilivyo uwepo wa watu wenye uelewa, wenye wema, haki na wanaopenda maridhiano,” amesema Guterres.

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kushirikiana kwa mustakbali bora wa wote.
Bwana Guterres amesema kwa kufanya hivyo ndio njia bora zaidi ya kuwaenzi wale waliopoteza maisha kwenye janga la mauaji ya kimbari nchini Rwanda miaka 25 iliyopita.