Ukatili wa kilichotokea Rwanda ni dhahiri kwingineko- Guterres

6 Aprili 2018

Siku ya Jumamosi ya tarehe 7 Aprili mwaka huu wa 2018 ni kumbukizi ya kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi mwanzoni mwa mwaka huu siku hii kutambuliwa kimataifa.

Miaka 24 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda bado ukatili wenye sura wa kile kilichotokea nchini Rwanda unaripotiwa maeneo mbalimbali duniani, umesema Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake wa kumbukizi ya mauaji hayo.

Katibu Mkuu Antonio Guterres ametaja ongezeko la matukio ya ubaguzi wa rangi, kauli za chuki na chuki dhidi ya wageni akisema vitendo hivi vinaweka mazingira bora ya kukua kwa maovu duniani.

Mathalani huko Mynamar, amesema waislamu wa kabila la Rohingya,  wanauawa, wanateswa, wanabakwa na hata kuchomwa moto wakiwa hai, matendo ambayo amesema ni kiashiria kuwa bado mataifa ulimwenguni hajayajifunza kutokana na kile kilichotokea Rwanda.

Wakati wa kumbukizi ya miaka 20 ya mauaji ya kimbari, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mwaka 2014. Picha ya Umoja wa Mataifa/Evan Schneider
Wakati wa kumbukizi ya miaka 20 ya mauaji ya kimbari, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mwaka 2014. Picha ya Umoja wa Mataifa/Evan Schneider

Bwana Guterres amesema ni wajibu wa nchi kuzingatia matamko  ya haki likiwemo lile la haki za binadamu na pia mkataba wa kimataifa wa kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari.

Amesisitiza kuwa kuokoa watu walio hatarini ni zaidi ya kutamka maneno, hivyo “ni lazima kujenga ujasiri wa kujali na kuazimia kuchukua hatua. Ni kwa kufanya hivyo tu ndio tutakuwa tunakumbuka vyema wahanga na manusura wa mauaji ya kimbari na kuhakikisha kitendo hicho katu hakirudii tena”, amesema Bwana Guterres.

Akizungumzia kumbukizi ya mauaji ya Rwanda na kile anachotaka kuona kinafanyika, Adama Dieng ambaye ni mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari amesema..

(Sauti ya Adama Dieng)

“Hatuwezi kuruhusu binadamu wauawe eti tu kwasababu ya vile walivyo. Hatuwezi kuruhusu binadamu wabaguliwe kwa sababu ya dini, kwa sababu ya kabila, utaifa au rangi yao.”

Katika siku 100 za ghasia nchini Rwanda mwaka 1994, zaidi ya watu 800,000 waliuawa wengi wao wakiwa ni watutsi, huku pia wahutu na watwa wenye msimamo wa kati nao pia walikumbwa na zahma hiyo.

TAGS: Rwanda, mauaji ya kimbari,

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter