Skip to main content

Hatua lazima zichukuliwe kukomesha mzunguko wa machafuko Mali:UN

Moja ya vijiji kwenye eneo la Mopti nchini Mali.
WFP/Alexandre Brecher-Dolivet
Moja ya vijiji kwenye eneo la Mopti nchini Mali.

Hatua lazima zichukuliwe kukomesha mzunguko wa machafuko Mali:UN

Tabianchi na mazingira

Hatua za haraka lazima zichukuliwe na jumuiya ya kimataifa kukomesha mzunguko wa machafuko ya kijamii na umwagaji damu unaoendelea nchini Mali machafuko ambayo hadi sasa yameshakatili maisha ya watu 160.

Wito huo umetolewa leo na mtaalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa mfululizo wa mashambulizi kwenye jimbo la Kati la Mopti yaliyofanyika Machi 23 yamefuatiwa na ghasia mpya Machi 26.

Mataalam huyo ambaye ni mahsusi kwa ajili ya hali ya haki za binadamu nchini Mali Alioune Tine amesema “Nimeshitushwa na machafuko haya mapya na nataka kutoa salamu zangu za rambirambi kwa waathirika na familia zao kutokana na mashambulizi haya ambayo yamefanyika kutokana na mivutano ya kijamii. Ni lazima kuwe na uchunguzi wa kina na wa haraka na wahusika ni muhimu kuhakikisha wanafikishwa mbele ya sheria.”

Amesema kulinda maisha ya watu  na mustakabali wa raia ni suala lililo njia panda hivi sasa, hivyo “natoa wito kwa vikosi vya usalama katika eneo hilo lakini pia majeshi ya serikali ya Mali na mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA kuimarisha juhudi zao ili kulinda raia.”

Amesisitiza kwamba ni muhimu sana kwa mivutano hii ya kijamii na mzunguko wa machafuko vikashughulikiwa haraka endapo tunataka kuepuka hatari ya uhalifu dhidi ya ubinadamu“natoa wito kwa Muungano wa Afrika AU na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS kuandaa mkutano ili kujaribu kusaka suluhu.”

Machafuko ya Machi 23 katika vijiji vya Ogossagou na Welingara jimboni Mopti yaliwajeruhi pia watu 70na katika shambulio moja la hatari Zaidi watu 150 wafugaji wa kabila la Fulani waliuawa na wanaodaiwa kuwa ni wajumbe wa kabila la Dogon.

Mtaalam huyo huru pia amearifiwa kwamba watu waliojihami kwa silaha wanaodaiwa kuwa ni wa kutoka kabila la Fulani walishambulia Kijiji Ouadou ambacho ni cha watu wa kabila la Dogon mnamo Machi 26 na kuua Wadogon 4 , na kuchoma moto nyumba kadhaa hali iliyowafanya watu wa eneo hilo kufungasha virago na kukimbilia vijiji vya jirani.

Katika shambulio lingine dhidi ya Wadogoni siku hiyohiyo kwenye eneo la Kere Kere lilisababisha kuuawa kwa wanawake wawili na wengine 20 kutekwa nyara. Kwa mujibu wa mtaalam Tine kinachomtia wasiwasi ni kuundwa wamakundi yenye silaha ya  makabila hayo kwa lengo la kujilinda “Kuongezeka kwa idadi ya makundi haya katika miaka minne iliyopita  ambayo baadhi ni ya itikadi kali , kusambaratisha mifumo ya asili ya kutatua migogoro , na uwepo mdogo wa mamlaka ya serikali ya Mali katika eneo hilo kumesababisha kuzorota kwa hali ya usalama ambayo umechangia ukiukwaji wa haki za msingi za watu wa jimbo la Mopti.”

Mataalam huyo amesema tangu Januari 2019 hadi sasa kumekuwa na matukio 22 ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaotekelezwa na makundi haya na kusababisha vifo vya watu takriban 230.

Adama Dieng naye aonesha wasiwasi. 

Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari Adama Dieng akizungumzia tukio la Machi 23 ameeleza kusikitishwa kwake na pia amelaani mauaji hayo yaliyotekelezwa katika Kijiji cha Ogossagou Peulh, huko Mopti katikati mwa Mali na akaonesha wasiwasi wake “katika miezi ya hivi karibuni, vurugu zimefikia kiwango cha juu katika mashambulizi ya kulipiza kisasi na ukikukwaji mkubwa wa haki za binadamu katikati mwa Mali hali iliyoziathiri jamii zote. Bila masuala haya kushughulikiwa mapema, kuna hatari ya hali kuwa mbaya zaidi.”