Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya raia nchini Mali yakome- Mtaalamu

Moja ya vijiji kwenye eneo la Mopti nchini Mali.
WFP/Alexandre Brecher-Dolivet
Moja ya vijiji kwenye eneo la Mopti nchini Mali.

Mashambulizi dhidi ya raia nchini Mali yakome- Mtaalamu

Haki za binadamu

Mashambulizi yanayoendelea kila uchao nchini Mali dhidi ya raia yanaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu na hivyo ni lazima hatua zichukuliwe kulinda raia na mali zao.

Hiyo ni kauli ya Alioune Tine, mtaalamu huru wa haki za binadamu kwa nchi ya Mali, kauli ambayo ametoa kufuatia shambulio la mwishoni mwa wiki kwenye kijiji cha Dogon huko Sabanou-Kou kwenye jimbo la Mopti nchini Mali.

Akinukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR mjini Geneva, Uswisi, Bwana Tine amesema “nimepokea ripoti ya kwamba watu wengi wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa huku makumi kadhaa wakitekwa, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.”

Amesema amejulishwa kuwa uchunguzi unaendelea kufanywa na mamlaka nchini Mali ikiwemo kufahamu idadi kamili ya waathirika wa tukio hilo, akisema, “taarifa zitatolewa punde.”

Mtaalamu huyo amesema shambulio hilo huko Sobanou-Kou la tarehe 9 mwezi huu wa Mei, ambalo liliendelea usiku kucha ni sehemu ya msururu wa mashambulio kwenye eneo la kati mwa Mali akisema, “mara nyingi yanafanywa dhidi ya raia.”

Mwanamke aliyefurushwa Kaskazini mwa Mali ukanda wa Sahel akiwa katika makazi ya muda karibu na kituo cha basi Mopti
UNDP/Nicolas Meulders
Mwanamke aliyefurushwa Kaskazini mwa Mali ukanda wa Sahel akiwa katika makazi ya muda karibu na kituo cha basi Mopti

“Kitendo cha wahalifu kuendelea kukwepa sheria, kinafanya watekelezaji wajione kuwa wana kinga, na ukiukwaji huu wa haki ambao kila wiki unaripotiwa kwa zaidi ya mwaka sasa unaweza kuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu,” amesema Bwana Tine.

Hata hivyo ameunga mkono hatua za haraka zilizochukuliwa na serikali ya Mali dhidi ya mashambulio hayo akitolewa mfano shambulio la tarehe mosi mwezi Januari mwaka huu na tarehe 23 mwezi Machi kwenye vijiij vya Fulani na maeneo mengine.

Ingawa hivyo amesihi mamlaka za Mali kuchukua hatua za kuzuia na kulinda raia ikiwemo kuimarisha ulinzi kwenye jimbo hilo la Mopti sambamba na kupokonya silaha vikundi vilivyojihami na kuchunguza watekelezaji wa mashambulio ili wafikishwe mbele ya sheria.

 Mtalaamu huyo pia amegeukia viongozi wa kijamii, kidini na kijadi na pia jamii ya kimataifa akiwasihi, watekeleze nao wajibu wao ili kulinda raia.