Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatupaswi kufumbia macho kinachoendelea Mali- Mtaalamu

Kundi la maafisa polisi wa UN waliopo ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, wakizungumza na raia wakati wa doria mjini Menaka, kaskazini mwa Mali.
UN /Marco Dormino
Kundi la maafisa polisi wa UN waliopo ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, wakizungumza na raia wakati wa doria mjini Menaka, kaskazini mwa Mali.

Hatupaswi kufumbia macho kinachoendelea Mali- Mtaalamu

Amani na Usalama

Mamlaka nchini mali lazima zichunguze kwa kina na kwa haraka ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, amesema mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Mali, Alioune Tine.

Katika taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi hii leo, Bwana Tine amesema wakati wa ziara yake aliyohitimisha nchini Mali, amepokea simulizi kutoka kwa waathirika na za kupitia vyombo vingine kuhusu mashambulizi yanayofanywa na wanamgambo wa kijadi kwa ushirikiano na vikundi vilivyojihami kwenye maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Mali.

“Watu kuuawa, kujeruhiwa, uharibifu au uchomaji moto wa mali za watu na watu hao kulazimisha kukimbia makazi yao ni miongoni mwa matokeo ya mashambulizi  hayo ,” amesema Bwana Tine.

Ametaja eneo la Ménaka akisema kuwa hali ya haki za binadamu huko pamoja na usalama na kibinadamu inazidi kutia hofu kubwa akitaka serikali ya Mali iazimie kuanza uchunguzi wa vitendo hivyo vya uhalifu ili watekelezaji wafikishwe mbele ya sheria.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo hadi mwisho wa mwezi Februari mwaka huu zaidi ya shule 657 zililazimika kufungwa kwenye maeneo ya kati na kaskazini mwa Mali kutokana na mashambulizi hayo na hivyo kuathiri zaidi ya wanafunzi 190,000

Doria ikiendelea kwenye mitaa ya mji wa Menaka, kaskazini mwa Mali. Msafara unajumuisha maafisa polisi wa UN, UNPOL na walinda amani kutoka Togo waliopo kwenye ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA.
MINUSMA/Marco Dormino.
Doria ikiendelea kwenye mitaa ya mji wa Menaka, kaskazini mwa Mali. Msafara unajumuisha maafisa polisi wa UN, UNPOL na walinda amani kutoka Togo waliopo kwenye ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA.

Jambo linalomsikitisha zaidi ni kwamba vitendo hivyo vya uhalifu dhidi ya raia vinafanyika kwenye maeneo ambako uwepo wa serikali ni dhaifu na hivyo makundi yenye misimamo mikali kushamiri na kutesa raia.

Bwana Tine ambaye alipata fursa pia ya kufika eneo la Mopti anasema alielezwa kuwa vikundi vyenye misimamo mikali kama vile Jama'at Nusrat al-Islam Wa al-Muslmeen, JNIM, vinanyanyasa jamii.
 
Amegusia pia ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanuwa na jeshi la Mali akimpongeza Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye alisema kuwa serikali katu haitovumilia uhalifu wowote ule dhidi ya raia.
 
Kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na kibinadamu nchini Mali, takribani watu milioni 4.1 wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Bwana Tine amesema kwa kinachoendelea sasa, “hii ni dharura ambayo hatuwezi kufumbia macho yetu. Vikundi vilivyojihami lazima viheshimu wafanyakazi wa kibinadamu na kazi yao ya kusaidia wale wenye mahitaji ya misaada pamoja na ulizi.”

Huku uchaguzi wa rais nao ukikaribia baadaye mwezi huu amesihi kuwa uwe huru, haki na uwazi na uzingatie vigezo vya kimataifa.

 
Wakati wa ziara hiyo, Bwana Tine alikutana na viongozi wa serikali ya Mali, wawakilishi wa mashirika ya kiraia ikiwemo wahanga wa mashambulizi, viongozi wa kidini na kijadi.
Ripoti yake ataiwasilisha mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwakani.
TAGS: Alioune Tine, Mali, Mopti,