Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimeshtushwa na vifo vya abiria wengi kwenye boti Iraq:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Nimeshtushwa na vifo vya abiria wengi kwenye boti Iraq:Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ameshtushwa na vifo vya abiria baada ya boti kuzama Alhamisi kwenye mto Tigris mjini Mosoul nchini Iraq.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika , serikali na watu wa Iraq kwa msiba huo na kuwatakia majeruhi ahuweni ya haraka.

Kwa mujibu wa duru za habari  kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Iraq waathirika wakubwa ni wanawake na Watoto na boti hiyo ilikuwa na takribani watu 200 waliokuwa wakielekea kwenye kisiwa cha utalii cha Umm Rabaen kama sehemu ya maadhimisho ya sherehe za kuanza msimu wa chipukizi au mwaka mpya kwa watu wa Iraq maarufu kama Nowruz.

Duru zinasema takribani Watoto 19 na wanawake 61 ni miongoni mwa watu 94 wanaodaiwa kupoteza maisha na 55 waliokolewa.  Imeelezwa kuwa idadi ya vifo ni kubwa sababu asilimia kubwa ya watu hao hawakuweza kuogelea.

Katibu Mkuu ameelezea mshikamano wa Umoja wa Mataifa na watu wa Iraq na dhamira yake ya kusaidia juhudi za kitaifa endapo zitahitajika.