Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya, WHO na Bloomberg wazindua mradi kupunguza vifo vya ajali za barabarani 

Barabara ya UN jijini Nairobi nchini Kenya iko wazi wakati huu ambapo watu wanafanyia kazi nyumbani kuepuka kusambaza virusi vya corona.
UN Kenya/Newton Kanhema
Barabara ya UN jijini Nairobi nchini Kenya iko wazi wakati huu ambapo watu wanafanyia kazi nyumbani kuepuka kusambaza virusi vya corona.

Kenya, WHO na Bloomberg wazindua mradi kupunguza vifo vya ajali za barabarani 

Masuala ya UM

Ajali za barabarani ni sababu ya tano kuu ya vifo vya Wakenya wenye umri wa kati ya miaka 5 na 70, na ni muuaji mkuu wa wavulana wenye umri wa miaka kati ya 15-19 limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO. 

Kwa kulitambua hilo leo mamlaka ya kitaifa ya uchukuzi na usalama, shirika la WHO na wahisani wa Bloomberg wamezindua mpango mpya wa kitaifa nchini Kenya wa kupunguza vifo na majeraha mabaya yatokanayo na ajali za barabarani kwa kuimarisha sheria, sera na hatua ambazo zimethibitishwa kuokoa maisha. 

Kenya ilirekodi vifo 4,579 kutokana na ajali za barabarani mwaka 2021, na makumi ya maelfu ya watu walijeruhiwa vibaya.  

Hadi kufikia tarehe 22 Mei 2022, vifo 1,816 zaidi vimerekodiwa, ikionyesha ongezeko la zaidi ya asilimia 9% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka wa 2021, kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka mamlaka ya kitaifa ya usafiri na usalama ya Kenya. 

Hakuna vifo vya ajali vinavyostahili 

Kwa mujibu wa Agnes Odhiambo, mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya kitaifa ya chukuzi na usalama “hakuna vifo vya ajali za barabarani vinavyokubalika  na ajali za barabarani ni suala la afya ya umma ambalo tunafanya kazi kwa bidii kulitatua haraka. Tunafanya kazi na WHO na washirika wengine kupitia mpango wa uhisani wa Bloomberg kwa ajili ya usalama barabarani  kote duniani ambao utakuwa muhimu katika kuunga mkono juhudi zetu za kuokoa maisha na kusukuma mbele mchakato.”  

Uzinduzi wa mradi wa Bloomberg nchini Kenya kwa ajili ya usalama barabarani duniani, umekuja wakati serikali inakamilisha mpango mpya wa kitaifa wa usalama barabarani ambao unalenga kupunguza nusu ya vifo kutokana na ajali ifikapo 2030.  

Serikali ya Kenya, WHO, wahisani wa Bloomberg na washirika wengine wanakutana kufafanua jinsi mpango huo unavyoweza kusaidia vyema mpango mpya wa serikali wa usalama barabarani. 

"Vifo vya ajali za barabarani nijanga ambalo linachificha mahali pa wazi. Kuongeza hatua za usalama barabarani ni muhimu, kwani pamoja na hali mbaya ya maisha ya binadamu, usalama barabarani unagusa maisha yetu yote kila siku, ikiwa ni pamoja na kufika kazini na shuleni. Kwa kuimarisha sheria, desturi na kuleta washirika pamoja, mradi wa wahisani wa Bloomberg ni muhimu katika kuokoa maisha,” amesema Dkt Abdourahmane Diallo, mwakilishi wa WHO nchini Kenya. 

Kila mwaka watu milioni 1.3 hufa kwa ajali za barabarani 

WHO inasema ulimwenguni kote, ajali za barabarani zinaua takriban watu milioni 1.3 kila mwaka ambapo ni watu zaidi ya wawili kila dakika huku zaidi ya vifo 9 kati ya 10 vyote vikitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati.  

Ajali za barabarani ndio sababu kuu ya vifo vya watoto na vijana wa umri wa kati ya miaka 5-29 ulimwenguni kote.  

WHO inakadiria kuwa ajali zitasababisha vifo vingine milioni 13 na majeruhi milioni 500 kote ulimwenguni kufikia mwaka 2030 ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa. 

Kelly Larson, anayeongoza mradi wa wahisani wa Bloomberg kwa usalama barabarani ulimwenguni amesema “Mradi wa wahisani wa Bloomberg unajivunia kushirikiana na serikali ya Kenya kuimarisha juhudi za usalama barabarani ambazo zitaokoa maisha. Tumejitolea kuunga mkono hatua zilizothibitishwa za usalama barabarani zinazookoa maisha.”  

Tangu mwaka 2007, mradi wa wahisani wa Bloomberg umeokoa maisha na kupunguza majeruhi wa kutokana na ajali za barabarani kwa kusaidia utekelezaji wa hatua za usalama barabarani katika miji na majimbo 45, kutetea sera thabiti za usalama barabarani katika nchi 21, na kuboresha viwango vya usalama wa magari katika masoko manne ya kanda.  

Juhudi hizi zinakadiriwa kuokoa maisha ya karibu  watu 312,000.