Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mwaka watu takribani laki 6.5 hufariki kutokana na homa ya mafua. WHO yazindua mkakati kabambe. 

Mtaalamu wa maabara akitafiti virusi vya mafua ya ndege katika maabala ya afya ya binadamu.
World Bank
Mtaalamu wa maabara akitafiti virusi vya mafua ya ndege katika maabala ya afya ya binadamu.

Kila mwaka watu takribani laki 6.5 hufariki kutokana na homa ya mafua. WHO yazindua mkakati kabambe. 

Afya

Leo mjini Geneva Uswisi shirika la afya duniani WHO limezindua mkakati wa mwaka 2019 hadi 2030 unaolenga kuwalinda watu duniani kote dhidi ya homa ya mafua na pia kuzuia virusi vya mafua kusambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amenukuliwa akisema, “tishio la janga la mafua lipo wakati wote. Hatari inayoendelea hivi sasa ya virusi vipya  vya mafua vinavyoambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na uwezekano wa kusababisha janga. Swali si kama tutakuwa na janga lingine, swali ni lini?Tunapaswa kukaa tayari na kujiandaa. Gharama ya kulipuka kwa homa ya mafua itakuwa kubwa zaidi kuliko ya kuzuia.”

Homa ya mafua inabaki kuwa moja ya changamoto kubwa kwa afya ya jamii ulimwenguni. Kila mwaka kote duniani, kunakadiriwa kuwa na maambukizi kwa watu bilioni moja, ambapo watu kati ya milioni 3 hadi 5 wanapata maambukizi makali yanayosababisha vifo kati ya 290,000 hadi 650,000. WHO inawashauri watu kupata chanjo ya kila mwaka dhidi ya homa ya mafua ikiwa ni njia muafaka ya kujikinga na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa WHO, mkakati huu mpya ni mkubwa zaidi kuwahi kufanywa na WHO dhidi ya homa ya mafua na utawafikia wengi.

Mpango huu unakusudia kuzijengea nchi uwezo imara wa kufuatilia ugonjwa na kuchukua hatua, kuzuia na kudhibiti pamoja na kujiandaa. 

“Kwa kazi ambazo tumekuwa tukifanya kwa ushirikiano na nchi, dunia imejiandaa vizuri kuliko wakati mwingine wowote dhidi ya mlipuko mkubwa ujao, lakini bado hatujajiandaa vya kutosha. Kimsingi, unahusu kuandaa mfumo wa afya kuweza kukabiliana na mshituko na hili linatokea pale ambapo mifumo ya kiafya iko imara” amesisitiza Dkt Tedros.

WHO inasema itapanua ushirikiano ili kuongeza utafiti, ubunifu na uwepo wa vitendea kazi vipya na vilivyoboreshwa ili kuzinufaisha nchi zote. Wakati huo huo, WHO itafanya kazi kwa ukaribu nan chi kuboresha uwezo wao wa kuzuia na kudhibiti homa ya mafua.