Ajabu wanawake 5 watwanga mtama kwa mlo mmoja, tubadilike- FAO

8 Machi 2019

Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani hii leo, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema kuwekeza kwa wanawake na wasichana ni hatua mujarabu katika kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2030. 

Afisa mwandamizi wa masuala ya jinsia, FAO Tacko Ndiaye akihojiwa mjini Roma, Italia amesema kuwekeza ni muhimu kwa sababu hivi sasa wanawake na wasichana walioko kwenye sekta hiyo wanakabiliwa na matatizo lukuki, huku watoto wengi wa kike wakikosa muda wa kujipambanua kielimu kutokana na kupoteza muda mrefu kusaka maji kwa ajili ya jamii zao.

Kama hiyo haitoshi ametaja teknolojia akisema “ni vigumu kuona wanawake watano wakitwanga mtama kwa saa mbili kwa ajili ya kuandaa mlo mmoja. Bila kushughulikia suala la teknolojia ili kupunguza mzigo wa kazi kwa wanawake ili waweze siyo tu kuongeza uzalishaji bali pia ubora wa mazao, hadhi ya mwanamke itaendelea kuwa ya chini.  Kwa sababu iwapo watatumia muda huo kutwanga mtama hawataweza kushiriki kwenye shughuli yoyote inayohusisha soko.”

Kwa mantiki hiyo afisa huyo mwandamizi wa jinsia FAO amesema ni lazima kuhakiksha ,“wanawake wakiwemo vijana wa kike wanaweza kupata na kumiliki ardhi, teknolojia, ubunifu, mikopo, fedha na pia wapate fursa za masoko ili waboreshe kiwango cha mazao wanayozalisha ili hatimaye waweze kuuza kwenye masoko ya hadhi ya juu duniani.”

Kwa mujibu wa FAO asilimia 45 ya nguvukazi kwenye sekta ya kilimo ni wanawake lakini wanakosa fursa na  haki sawa za kiuchumi na kijamii kama ilivyo kwa wanaume.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter