Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu mpya kusaidia watu kubaini uwezo wao wa kusikia

Mebratu almaarufu Tanki ni mvulana wa miaka 16 kutoka Eritrea. Muziki ni moja ya vitu anavyopenda, anapenda kusikiliza nyimbo za kitamaduni kupitia vipokea sauti vinavyobanwa kichwani.
© UNICEF/UN0264259/Haro
Mebratu almaarufu Tanki ni mvulana wa miaka 16 kutoka Eritrea. Muziki ni moja ya vitu anavyopenda, anapenda kusikiliza nyimbo za kitamaduni kupitia vipokea sauti vinavyobanwa kichwani.

Apu mpya kusaidia watu kubaini uwezo wao wa kusikia

Afya

Kuelekea siku ya kimataifa ya usikivu wa sikio tarehe 3 mwezi huu wa Machi, shirika la afya ulimwenguni, WHO limezindua apu inayoweza kusaidia watumiaji wa simu za kiganjani kuweza kubaini kiwango cha usikivu wa masikio yao.

Apu hiyo ikiwa imepatiwa jina “hearWHO” inapakuliwa bure kwa ajili ya watumiaji wa simu za kiganjani ambapo itasaidia wale ambao tayari wana shida ya usikivu au wako hatarini kupoteza uwezo wao wa kusikia.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kuwa  apu hiyo inatumia tarakimu za kiwango cha sauti kinachokubalika ambapo mtumiaji anatakiwa aweke msururu wa tarakimu tatu pindi anapotakiwa kufanya hivyo.

Tarakimu hizo zinaambatana na sauti katika  viwango mbalimbali vyenye mazingira tofauti ya kila siku na kumpatia kiwango cha mtumiaji, ambapo WHO inasema mtumiaji anaweza kujipima kila siku.

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Etienne Krug amesema kitendo cha mtu kuweza kupima uwezo wake wa usikivu kitasaidia mtu kubaini mapema iwapo yuko hatarini au la.

Dkt. Krug amesema watu wengi waliopoteza uwezo wa kusikia hawafahamu hali hiyo na kwa mantiki hiyo basi wanapoteza fursa mbalimbali iwe ya elimu, ajira na hata nyinginezo za maisha.

Amesema uchunguzi wa mara kwa mara utasaidia tatizo kufahamika na hatua mahsusi kuchukuliwa haraka iwezekanavyo.

Hatua hizo ni pamoja na kuhamasisha watu kupunguza vitendo vinavyochochea kupoteza usikivu kama vile kusikiliza kitu kwa sauti kubwa kupita kiasi, matumizi ya lugha za alama, vifaa vya kusaidia mtu kuongeza uwezo wa kusikia na vipandikizi vya kumwezesha mtu kusikia ambapo WHO imesema hatua hizo zina nafuu.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 5 ya wakazi wa dunia sawa na watu milioni 466 wamepoteza uwezo wa kusikia ambapo kati yao hao, milioni 432 ni watu wazima na milioni 34 ni watoto.

Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050, zaidi ya watu milioni 900 au mtu mmoja kati ya watu 10 atakuwa amepoteza uwezo wa kusikia na duniani kote tatizo la watu kushindwa kusikia linagharimu dola bilioni 750 kila mwaka.