Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu za kwenye simu zachangia katika kudhibiti COVID-19- Dkt. Tedros

Mhudumu wa Afya nchini Madagascar akiwahudumia raia
World Bank/Henitsoa Rafalia
Mhudumu wa Afya nchini Madagascar akiwahudumia raia

Apu za kwenye simu zachangia katika kudhibiti COVID-19- Dkt. Tedros

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ametaja bara la Ulaya na Amerika kama maeneo ambako maambukizi mapya ya ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 yameripotiwa kwa kiasi kikubwa, hususan katika siku nne zilizopita.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Dkt. Tedros amesema katika miji mingi kwenye mabara hayo idadi ya wagonjwa wanaosaka matibabu hospitali sambamba na wale walio mahututi imeongezeka.

“Katu duniani haijawahi kutokea kuwa kuwepo kwa idadi kubwa ya wagonjwa kunawezesha kujenga kinga dhidi ya maradhi haya ya mlipuko, na usizungumzie kabisa ugonjwa ambao ni janga. Hii kisayansi na kimaadili ni tatizo. Kuruhusu virusi hatari ambavyo hata bado hatuvielewa, kuenea kwa uhuru ni kinyume na maadili. Hii siyo njia bora kabisa,” amesema Dkt. Tedros wakati huu ambapo baadhi ya nchi zinadai kuwa kuachilia idadi kubwa ya raia wake kuugua ndio njia pekee ya kujenga kinga dhidi ya Corona.

Amesema mbadala upo na kuna nchi ambazo zimechukua hatua kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona na hivyo kuokoa maisha.

Dkt. Tedros ametolea mfano teknolojia za kisasa za kudhibiti kusambaa kwa ambazo amesema zinaunga mkono mbinu za afya ya umma za kudhibiti Corona.

Mathalani apu ya kuonya kuhusu Corona, Corona Warn-app ambayo inatumika nchini Ukerumani kusambaza majibu ya vipimo vya Corona kwa watu waliopimwa. “Apu  hiyo katika simu 100 za mwanzo wa kutumika, imesambaza majibu kwa watu milioni 1.2.” amesema Dkt. Tedros.

Halikadhalika apu ya Aarogya Setu ya nchini India ambayo nayo pia inapatikana kwenye simu na imeshapakuliwa na watumiaji milioni 150, “imesaidia idara za afya kubaini maeneo ambako kuna uwezekano wa mlipuko na kupeleka huduma za vipimo.”

Nchini Denmark nako, kupitia apu ya kwenye simu, zaidi ya watu 2700 wamechunguzwa iwapo wana virusi vya Corona au la baada ya kupokea taarifa kupitia simu zao.
Nako nchini Uingereza, serikali imezindua apu mpya kuhusu COVID-19  ya Idara ya Afya nchini humo ambayo ndani ya wiki moja imepakuliwa zaidi ya mara milioni 10.

Pamoja na kuwajulisha watumiaji wake iwapo wamenaweza kuwa wameambukizwa virusi vya Corona, apu hiyo inaruhusu mtumiaji kupanga muda wa kufanyiwa uchunguzi na kupokea majibu, na kufuatilia pia maeneo ambayo walitembelea sambamba na kupokea maonyo mapya.

Dkt, Tedros amesema kwa sasa, WHO inashirikiana na kituo cha Ulaya cha kinga na udhibiti wa magonjwa ili kutathmini ufanisi wa apu zao za ufuatiliaji waambata wa wale wanaothibitishwa kuwa na virusi vya Corona.

Hadi sasa zaidi ya watu milioni 1 wamefariki dunia ulimwenguni kote kutokana na COVID-19 kati ya zaidi ya milioni 37 waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huo.