WHO yalaani shambulizi dhidi ya wahudumu wa afya Iraq
Shirika la afya duniani (WHO) limelaani vikali shambulio la hivi karibuni dhidi ya muhudumu wa afya ambaye alishambuliwa wakati akitoa huduma kwamgonjwa mahtuti ajuza wa miaka 70 katika Hospitali ya Azadi iliyopo katika jimbo la Kirkuk mapema nchini Iraq tarehe 18 mwezi huu.
Dk. Adham Rashad Ismail, ambaye ni kaimu mratibu wa WHO Iraq amesema "Mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kuwanyima idadi kubwa ya watoto, wanawake na wazee haki zao za huduma muhimu ya afya zinayotolewa na shirika hilo.”
Takwimu za WHO, zimebaini kuwa wahuduma katika vituo vya afya nchini Iraq wamekuwa wakishambuliwa tangu mgogoro ulivyongezeka mwaka 2014. Mnamo 2018 pekee, mashambulizi 42 yalirekodiwa na WHO Iraq, na asilimia 40% kati ya hayo ni dhidi ya wahudumu wa afya nchini
WHO inatoa wito kwa mamlaka nchini humo kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na wa wahudumu wa afya katika vituo mbalimbali vya afya, wakati huu ambapo idadi kubwa ya watu wakiwemo wakimbizi wa ndani , jumuiya za wenyeji na wahamiaji wanaendelea kuhitaji huduma muhimu, za kuokoa maisha, na pia kuhakikisha wagonjwa na vituo vya afya vinalindwa.