Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO kuanza kampeni ya chanjo dhidi ya dondakoo kwa wakimbizi wa Rohingya

Familia geni ya wakimbizi kutoka Myanmar wanasimama kwenye matope nje ya kambi ya wakimbizi ya Kutupalong. Picha:UNHCR

WHO kuanza kampeni ya chanjo dhidi ya dondakoo kwa wakimbizi wa Rohingya

Shirika la afya ulimwenguni WHO leo llimetangaza kuzindua kampeni kubwa ya chanjo ili kusitisha kusambaa kwa maradhi ya kupumua miongoni mwa wakimbizi wa Rohigya walioko Cox Bazar nchini Bangladesh.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva hii leo Fadela Chaib msemaji wa WHO amesema hadi kufikia siku mbili zilizopita kuna wakimbizi sita waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa dondakoo na visa zaidi ya 110 vilivyoambukizwa ugonjwa huo.

Amesema WHO inashirikiana na serikali ya Bangladesh , wizara ya afya ya nchi hiyo na washirika wengine kuhakikisha wanadhibiti kuenea kwa ugonjwa huo unaoambukiza kwa kasi kwa kutoa matibabu na kinga kwa wakimbizi hao.

Ameongeza kuwa kampeni itadumu kwa wiki mbili na inaanza Jumapili wiki hii , na inafanyika kwa msaada mkubwa wa India ambapo taasisi ya serum India imetoa dozi laki tatu za chanjo kwa ajili ya kampeni hiyo.