Dola milioni 122 zitawasaidia wakimbizi wa ndani na wanaorejea Sudan Kusini-IOM

5 Februari 2019

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM leo mjini Juba nchini Sudan Kusini, limezindua ombi lake la mwaka huu wa 2019 la dola milioni 122 zinahitajika ili kuwasaidia takribani watu milioni 1 nchini Sudan Kusini hususani wale ambao wamepoteza makazi na kujikuta katika ukimbizi wa ndani pamoja na wale wanaorejea baada ya kuyakimbia machafuko.

Tangu kuanza kwa mgogoro mwaka 2013, Sudan Kusini imekuwa ikikumbwa na changamoto za migogoro ya kibinadamu. Kwa zaidi ya miaka mitano zaidi ya watu milioni 4 wameyakimbia makazi yao wakitafuta usalama. Zaidi ya watu milioni 2 ni wakimbizi wa ndani.

Mkataba wa makubaliaono ya kumaliza mgogoro uliotiwa saini mwezi septemba mwaka jana 2018 unaleta matumaini ya amani jambo ambalo linafanya kuwepo watu wengi wanaorejea nchini humo.

Jean-Philippe Chauzy ambaye ni mkuu wa IOM nchini Sudan Kusini anasema, “tunahitaji kuwasaidia watu wa Sudan Kusini wakati nchi inapotafuta amani na mstakabali imara. IOM imekuwa ikitekeleza miradi ya mbalimbali ya kipindi cha mpito tangu Sudani Kusini ilipokuwa nchi mwaka 2011. IOM inatambulika kama mshirika wa kuaminika na kutumainiwa”

Miaka mingi ya vita imeendelea kuwaathiri zaidi ya watu milioni 7 ambao kwa haraka wanahitaji misaada na kulindwa. Ingawa ukubwa wa mgogoro umepungua  tangu mkataba wa amani ulipofikiwa lakini nchi bado inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu na gharama za mgogoro wa muda mrefu.

IOM ikiwa na zaidi ya wafanyakazi 2,350 ina ofisi zake mjini Juba, Wau, Bentiu, Malakal, Bor, Rumbek, Abyei na pia wana mawasiliano katika maeneo mengine kama Mangwi, Mayom, Kapoeta, Twic na Yei.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter