Zerrougui asifu ukomavu wa wananchi wa DRC

31 Januari 2019

Mwakilshi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC  Leila Zerrougui amepongeza ukomavu wa raia wa nchi hiyo uliofanikisha uchaguzi mkuu nchini humo na hatimaye Rais mpya Felix Tshisekedi kuapishwa na kuanza rasmi awam yake ya uongozi wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa, Bi. Zerrougui amesema, “nafikiri tulishuhudia historia katika nchi yenu. Tumeshuhudia pamoja nyakati ngumu, wasiwasi, hofu kuhusu nini kitatokea, kesho itakuwa vipi,” amesema mwakilishi huyo.

Ameongeza kuwa, “nadhani raia wa DRC wameonyesha ukomavu wa hali ya juu. Wamekuwa wavumilivu na wawakilishi wao na taasisi zao.”

Kwa mujibu wa Bi. Zerrougui, mazingira hayo yaliyoshuhudiwa  ya ukomavu yanasaidia wananchi wa DRC kujenga msingi wa taifa lao.

Bi. Zerrougui ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC amewaeleza waandishi hao wa habari kuwa wiki iliyopita alikuwa na mazungumzo na Rais Tshisekedi na kumwelezea utayari wa  Umoja wa Mataifa kusaidia serikali kwa kuzingatia vipaumbele vitakavyowekwa na taifa hilo.

Halikadhalika amesema alikutana pia na mgombea urais aliyehoji matokeo ya urais, Martin Fayulu na kumweleza kuwa ni muhimu kuendelea na dhima kama ya Bi. Zerrougui ya kushirikiana na wadau wote DRC na kusaidia kuwa na upinzani wenye dhima chanya.

Mwakilishi huyo wa UN nchini DRC anasema ni matumaini yake kuwa mwaka 2019 utakuwa mwaka wa utulivu, umoja na kuanza ujenzi wa mustakabali bora wa taifa hilo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud