Licha ya hatu zilizopigwa bado kuna changamoto kwenye mchakato wa uchaguzi DRC:Zerrougui

27 Agosti 2018

Kuna hatua zinazoonekana katika mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, hata hivyo mchakato wa uchaguzi huo unaotarajiwa Desemba 23 mwaka huu umeghubikwa na mgongano na mashauriano makali ya kisiasa.

Hayo yameelezwa leo na Leila zerrougui mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUCO wakati akitoa taarifa kwa njia ya video hii leo kuhusu mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa nchini DRC kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Bi. Zerrougui, amezichagiza pande zote katika mchakato huo kuendelea na majadiliano ili kuhakikisha mazingira stahiki yanawezeshwa kufanyika kwa uhuru na amani uchaguzi huo utakapowadia.

Amewaambia wajumbe wa Baraza kwamba uaminifu unaoonekana katika mchakato wa uchaguzi unasalia kuwa jambo muhimu, na hilo linaweza kupunguza mvutano uliopo nchini huko.

Suala la haki katika mchakato wa uchaguzi

Ameongeza kuwa kujumuishwa kwa wanawake zaidi katika mchakato wa uchaguzi pia ni suala la kupewa kipaumbele, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa hakuna vitisho dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu.

Bi Zerrougui pia amemetoa wito wa kuondolewa marufuku ya maandamano ya umma na kuunga mkono uhuru wa kujieleza na mikutano ya amani, ambayo amesema ni muhimu kufanya mchakato mzima kuleta maana hasa maendeleo mazuri wakati  huu uchaguzi ukikaribia.

 

MONUSCO/John Bompengo
Viongozi wa wanawake DRC wakiwakilisha sekta zote za asasi za kiraia, wakiwa na Leila Zerrougui, Mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO

 

Kuhusu hali ya Kibinadamu

Kuhusu hali ya kibinadamu amesema kwa mujibu wa mashirika ya misaada hali bado ni tete na inayotoa hofu hususan kwenye eneo la Uvira,kwenye jimbo la Kivu Kusini ambako watu zaidi ya 14,000 wametawanywa kufuatia shambulio lililofanywa na muungano wa wanamgambo wa Mai Mai Agosti 18. Watu wengi waliotawanywa na shambulio hilo wamelazimika kukimbia tena makwao.

Mapema mwezi huu watu wapatao 3,900 waliarifiwa kutawanywa katiika eneo la Shabunda na wengine 3,200 Kusini Mashariki mwa jimbo la Maniema kutokana na mapigano baina ya makundi yenye silaha na vikosi vya serikali.

Na tangu mwezi Juni Umoja wa Mataifa na washirika wake wamekuwa wakiwasaidia watu Zaidi ya 600,000 wanaohitaji msaada nchini DRC, wakiwemo wakimbizi wa ndani na wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi. Takriban watu 28,000 kati yao wako katika jimbo la Kivu Kusini.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud