Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inahitaji madini,  ajira za viwandani, mafunzo na maendeleo- rais Tshisekedi

Félix Antoine Tshilombo Tshisekedi, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakati wa hotuba yake kwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74
UN Photo/Cia Pak
Félix Antoine Tshilombo Tshisekedi, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakati wa hotuba yake kwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74

Dunia inahitaji madini,  ajira za viwandani, mafunzo na maendeleo- rais Tshisekedi

Amani na Usalama

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC inauhitaji Ujumube wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO lakini inahitaji MONUSCO iliyo haraka kutekeleza wajibu wake, ulio na vifaa, ulio  thabiti na ambao una wajibu sahihi, amesema rais wa DRC, Felix Tshisekedi katika hotuba yake ya kwanza kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Leo Alhamisi Septemba 26.

Katika hotuba hiyo kwenye mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74 rais Tshisekedi ambaye alichaguliwa kuwa rais Januari mwaka huu wa 2019 amesema, mtazamo wake na ule wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres unashabihiana kuhusu, “haja ya haraka ya MONUSCO kurekebisha muundo wake  kuendana na hali ya sasa mashinani, kwa kujikita zaidi na uwezo wa vikosi vya Umoja wa Mataifa kuendesha operesheni za uingiliaji kati bega kwa bega na vikosi vya DRC.”

Rais Tshisekedi ameongeza kwamba DRC ni mmiliki wa asilimia 47 ya misitu katika bara la Afrika na kwamba, “tumedhamiria kulinda misitu yetu. Hatahivyo uhifadhi wa urithi wetu wa asili hauwezi kufanyika katika hatari ya kukosa maendeleo.”

Aidha ameongeza, “haieleweki kwamba misitu ya Kongo ambayo ni misitu iliyotunzwa zaidi duniani  hupokea asilimia moja tu ya ufadhili.Ni muhimu kwa mashirika ya kifedha ikiwemo shirika la fedah duniani katika nafasi yake ya uongozi kwa ajili ya ufadhili wa maendelelo, kujumuisha maswala ya mazingira katika uchanganuzi wa mipango na changamoto za kiuchumi wakati wakisaidia nchi mbali mbali."

Rais Tshisekedi amesema, “leo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina asilimia 70 ya hifadhi ya mawe yenye madini kote duniani ambayo ni muhimu kwa ajili ya mabadiliko ya kawi na kidijitali ambayo wanadamu wanapitia kwa sasa.”

Mbali ya hayo amesema “badala ya kutumia raslimali hizo za asili kujipatia faida binafsi, nchi yake itafungua milango kwa dunia kuwezesha utaratibu wa kuchimba madini kwa kubadilishana na ukuaji wa viwanda na uzalishaji wa betri na vifaa vingine vya gharama.”

Akisisitiza kwamba, “dunia inahitaji kobalti, coltan na lithiamu. Tunataka ajira za viwanda, mafunzo na maendeleo.”