Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati wa mauaji tuliizoea mikokoteni iliyojaa maiti- Manusura wa mauaji ya wayahudi

Inge Auerbacher akisimulia alivyonurika  mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi wakati wa Vita Vikuu vya pili vya dunia.
UN /Loey Felipe
Inge Auerbacher akisimulia alivyonurika mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi wakati wa Vita Vikuu vya pili vya dunia.

Wakati wa mauaji tuliizoea mikokoteni iliyojaa maiti- Manusura wa mauaji ya wayahudi

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kumbukizi ya kuwaenzi waliopoteza maisha na manusura wa mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi yaliyotokea wakati wa Vita Vikuu vya pili vya dunia ameyaita mauaji hayo kuwa ni ya kikatili na ya kutisha kupindukia. 

Kumbukizi hiyo imefanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambapo pia manusura wamehudhuria.

Guterres amesema ingawa mauaji hayo yaliyowalenga wayahudi yalitokea miaka mingi iliyopita, lakini “kote duniani tunaona kuongezeka kwa namna nyingine za ubaguzi. Mashambulizi dhidi ya waislamu katika jamii kadhaa yameongezeka wakati mwingine yakizipita hata aina nyingine za chuki. Warohingya, wayazidi na wengine wengi wamekumbana na unyanyasaji kwa sababu tu ya dini au kabila zao.”

Guterres pia ameitumia nafasi hii kuwaonya baadhi ya wanasiasa ulimwenguni kote ambao wanahamasisha matendo mabaya kwa wafuasi wao akisema kuwa siku za nyuma walikuwa wanahamasisha mambo mabaya kwa siri lakini sasa wanasema waziwazi.

Amina Hassan/UNSocialMedia
Chuki! Chuki! Chuki! zimezidi sasa kuliko wakati wowote ule!

Naye Inge Auerbacher manusura wa mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi ambayo wakati yanatokea alikuwa na umri wa miaka 7 amewasimulia waliohudhuria akikumbuka masaibu aliyopitia na wenzake ambao wengi hawakuweza kuiona kesho yao.

Amesema “tulifikia wakati tukaizoea mikokoteni iliyojaa maiti. Mara tatu kwa siku tulisimama katika misururu mirefu tukiwa tumebebeba sahani zetu za chuma ili kupata mgao wetu wa chakula. Njaa, umati mkubwa, uchafu, chawa, panya, nzi, kunguni, na hofu ya kupelekwa mashariki vilitutesa kila siku.”

 Historia inasema wayahudi milioni 6 waliuawa  katika mauaji hayo ya halaiki yaliyotekelezwa na manazi wa kijerumani na kumbukizi ya mauaji hayo hufanyika tarehe 27 kukumbuka siku ambayo kambi ongozi ya mauaji hayo ya Auschwitz-Birkenau huko Poland ilipokombolewa.