Skip to main content

Tufundishe watoto upendo kabla wengine hawajafundisha chuki- Guterres

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) na Rabbi Arthur Schneier wa sinagogi la Park East jijini New York, Marekani ambako leo 26 Januari 2019 amehudhuria ibada ya kumbukizi ya mauaji ya halaiki.
Laura Gelbert / UN
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) na Rabbi Arthur Schneier wa sinagogi la Park East jijini New York, Marekani ambako leo 26 Januari 2019 amehudhuria ibada ya kumbukizi ya mauaji ya halaiki.

Tufundishe watoto upendo kabla wengine hawajafundisha chuki- Guterres

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umesema katu hauotasahau kile kilichowakumba wayahudi milioni 6 na mamilioni wengine waliouawa wakati wa mauaji ya halaiki.
 

Kauli hiyo ni ya Katibu Mkuu wa chombo hicho, Antonio Guterres ambayo ametoa leo jijini New York, Marekani wakati akishiriki ibada kwenye sinagogi la wayahudi, kukumbuka wayahudi waliouawa.

Kumbukizi hii inakwenda sambamba na siku ya kimataifa ya kumbukizi ya mauaji ya halaiki tarehe 27 Januari ambayo ni kukumbuka kukombolewa pia kwa kambi ya kifo ya Auschwitz-Birkenau huko Poland, ambayo ilitumiwa na manazi kuua wayahudi.

Guterres amesema “katu hatutoacha kuwa macho kuangalia viashiria vya mauaji ya kimbari katika zama za sasa. Na tutaendelea kuwa mstari wa mbele kupiga vita chuki dhidi ya wayahudi na kuimarisha chochote kile tufanyacho kulinda utu wa binadamu kwa wote.”

Amesema hatua hizo ni muhimu zaidi hivi sasa ambapo bado chuki dhidi ya wayahudi inazidi kushamiri akisema, “matukio ya chuki dhidi ya wayahudi kwa Marekani yaliongezeka kwa asilimia 57 mwaka 2017. Kura moja ya maoni huko Ulaya ilionyesha mwaka jana kuwa asilimia 28 ya wayahudi wamekumbwa na ukatili kisa tu wao ni wayahudi.”


Guterres anasema alichukizwa zaidi baada  ya kutambua kuwa kura ya maoni ya hivi karibuni barani Ulaya ilibaini kuwa theluthi mmoja ya watu walisema wanahafamu kidogo sana au hawafahamu kabisa kuhusu mauaji ya halaiki.

“Miongoni mwa waliozaliwa miaka ya 2000, theluthi mbili hawafahamu kabisa kambi ya kifo cha Auschwitz,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa kadri idadi ya manusura wa mauaji ya halaiki inavyopungua, ni jukumu la kila mtu  kusongesha ushuhuda wao kwa vizazi vijavyo.

Amesema kadri chuki inavyoenea siyo tu dhidi ya wayahudi bali pia waislamu na wageni, mitando ya kijamii nayo ikitumika kusaka wafuasi wa kueneza chuki hizo, elimu ni muhimu.

“Ni lazima kufundisha watoto upendo kabla watu wengine hawajawafundisha chuki. Umoja wa Mataifa umejizatiti kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza jukumu hilo. Mradi wetu wa kuelimisha mashinani kuhusu mauaji ya halaiki unatekeleza shughuli kadhaa kwenye makumi ya nchi,” amesema Katibu Mkuu.

Kesho ndio kumbukizi yenyewe ya siku ya kimataifa ya mauaji ya halaiki lakini Umoja wa Mataifa utakuwa na tukio maalum Jumatatu ya tarehe 28 Januari kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la chombo hicho.