Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuki dhidi ya wayahudi yaongezeka, tuchukue hatua: Guterres

Katu tusiwasahau
UN
Katu tusiwasahau

Chuki dhidi ya wayahudi yaongezeka, tuchukue hatua: Guterres

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kumbukizi ya mwaka huu ya mauaji ya halaiki inakuja wakati ambapo kuna ongezeko la chuki dhidi ya wayahudi.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo tarehe 27 Januari 2019, Guterres ametaja matukio tofauti ya kudhihirisha kauli hiyo kuanzia “shambulizi baya zaidi kwenye sinagogi nchini Marekani hadi utiaji najisi kwenye makaburi ya wayahudi huko Ulaya, chuki hii iliyodumu karne na karne siyo tu inazidi kuongezeka bali hali yake inakuwa mbaya.”
 
Amesema “tunashuhudia kuenea kwa vikundi vya Unazi-mamboleo na majaribio ya kuandika upya historia ili kuficha ukweli kuhusu mauaji ya halaiki. Tunashuhudia ukosefu wa stahamala ukishamiri kwa kasi kubwa kwenye intaneti.”
 
Katibu Mkuu ametanabaisha kuwa kadri muda wa Vita Vikuu vya Pili vya dunia unavyoyoyoma, na idadi ya manusura wa mauaji yahalaiki inapungua, “ni jukumu letu kuwa makini. Kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa wayahudi huko Uingereza, Jonathan Sacks, alivyosema: “Chuki inayoanza na wayahudi katu haitamatikii kwa wayahudi.”
 
Amesema bayana kuwa dunia hivi sasa inashuhudia ukosefu wa stahamala ukiingia kwenye siasa – ukilenga makundi ya wachache, waislamu, wahamiaji na wakimbizi, na kujinufaisha na hasira na hofu kwenye dunia hii inayobadilika.
 
Kwa mantiki amesema “sasa kuliko wakati wowote ule, hebu na tuungane kupigania kurejesha maadili ya kimataifa na kujenga dunia yenye usawa kwa wote.”

Jua likizama katika kambi ya Auschwitz-Birkenau walikopata mateso wayahudi.  Kambi hii iliyopo Poland imesalia kuwa ishara ya ugaidi, mauaji ya kimbari na ya holocaust.
UN / Evan Schneider
Jua likizama katika kambi ya Auschwitz-Birkenau walikopata mateso wayahudi. Kambi hii iliyopo Poland imesalia kuwa ishara ya ugaidi, mauaji ya kimbari na ya holocaust.

Siku ya leo inalenga kukumbuka wayahudi milioni sita ambao waliteketea kwenye mauaji ya halaiki—na manusura wengine wengi wa ukatili uliopangwa na wa kutisha.