Skip to main content

Si vioo tu vilivunjwa wakati wa ‘Kristallnacht’ bali pia familia na ndoto- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza katika makumbusho ya urithi wa wayahudi jijini New  York, Marekani wakati wa kumbukizi ya 81 ya mauaji ya Kristallnacht.
UN/Antonio Ferrari
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza katika makumbusho ya urithi wa wayahudi jijini New York, Marekani wakati wa kumbukizi ya 81 ya mauaji ya Kristallnacht.

Si vioo tu vilivunjwa wakati wa ‘Kristallnacht’ bali pia familia na ndoto- Guterres

Amani na Usalama

Miongo kadhaa baada ya mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi,  chuki hiyo iliyodumu zaidi duniani bado imesalia ulimwenguni.

Hiyo ni kauli ya  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres aliyotoa hii leo kwenye makumbusho ya urithi wa kiyahudi yaliyoko jijini New York, Marekani, ambako kumefanyika kumbukizi ya siku ya mauaji ya wayahudi yaliyofanywa na manazi wa Ujerumani na kupatiwa jina la Kioo kilichovunjwa.

Mauaji hayo yalifanywa na wanamgambo wa kinazi kuanzia tarehe 9  hadi 10 mwezi Novemba mwaka 1938 kwenye maeneo yaliyokuwa chini ya manazi wa kijerumani ambapo utawala wa kijerumani hawakuchukua hatua yoyote kulinda na nyumba zilishambuliwa na vioo kusambaa maeneo mbalimbali barabarani.

Bwana Guterres amesema usiku huo wa kioo kilichovunjwa au Kristallnacht, haukuwa tu usiku wa kuvunja vioo bali pia kuvunja maisha ya watu, kuvunja familia, kuvunja jamii na kuvunja ndoto za watu.

Baada ya kutazama picha za maonyesho hayo yaliyopatiwa jina Si zamani sana. Si mbali sana” Katibu Mkuu amesema ni kumbusho ya kwamba chuki, chuki dhidi ya wayahudi na mauaji ya halaiki hayakufanyika zamani sana na hayako mbali sana.

Kwa hiyo, maonyesho  haya kwa kweli siyo tu ni fursa ya kutazama tulipotoka, bali yanatusaidia kutathmini nyakati za sasa na kutambua umuhimu wa kuendelea kuwa macho,” amesema Katibu Mkuu.

Amesema  kuwa macho ni muhimu kwa sababu katika miezi ya hivi karibuni pekee, dunia kote kumeshuhudiwa uharibifu wa makaburi ya mayahudi, kupakwa kinyesi kwa kumbukizi ya mauaji ya halaiki, kuchomwa moto kwa Yeshiva na kuenezwa kwa propaganda za hovyo dhidi ya wayahudi.

Bwana Guterres amesema chuki inazidi kuota mizizi pia kwani baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaleta maoni ya hovyo ya vikundi vyenye misimamo mikali na hii inafanyika katika tawala za kibabe na pia kwenye nchi zenye demokrasia.

Watoto wakiwa wamevalia tisheti zenye ujumbe wa kuungana dhidi ya chuki, wakati wa kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi.
UN Photo/Rick Bajornas)
Watoto wakiwa wamevalia tisheti zenye ujumbe wa kuungana dhidi ya chuki, wakati wa kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi.

Mitandaoni nako hali si shwari

Amegusia pia mitandaoni ambako amesema vikundi vya unazi mamboleo na misimamo mikali inasambaza ujumbe wa kilaghai unaolenga jamii zilizo hatarini kudanganywa huku wakiahidiwa neema.

“Wazazi, walimu na viongozi wa kisiasa, lazima sote tuchukue hatua ya dharura kabla chuki za kichinichini hazijaibuka na kuleta hali ya tashwishwi,” amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha kuwa Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko kidete kukabiliana na hali hiyo kwa kuwa “mwezi Juni nilizindua mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kukabili na kushughulikia kauli za chuki.”

Halikadhalika amesema elimu ni msingi mkuu wa kuzuia kauli za chuki “na ninatangaza leo kuwa nina nia ya kuitisha mkutano juu ya nafasi ya elimu katika kushughulikia na kujenga mnepo dhidi ya kauli ya chuki.”

Guterres pia akataja mpango wa utekelezaji waliozindua miezi miwili iliyopita kusaidia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha waumini wanaabudu bila bughudha.

Bwana Guterres amesema kuwa watu hawazaliwi kujenga chuki, na kwamba stahamala inafundishwa na vivyo hivyo inaweza kuzuia na isisomwe.