Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UNIDO waleta nuru kwa wakulima wa ndizi Uganda

Ndizi
Picha: World Bank/Yosef Hadar
Ndizi

Mradi wa UNIDO waleta nuru kwa wakulima wa ndizi Uganda

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO linasaidia jamii zilizoko hatarini magharibi mwa Uganda kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa fursa zaidi ili kuweza kupata kipato, kupunguza umaskini na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa kutumia mbinu za kuboresha zao la ndizi.

Maeneo ya magharibi na kusini magharibi mwa Uganda yanajivunia katika uzalishaji wa ndizi ambazo zinavunwa na kusafirishwa hata nje ya nchi. Licha ya kwamba zao hilo lina umuhimu mkubwa kama lishe, lakini vipato kutokana na mauzo yake ni vya chini kama anavyoelezea Rebecca Nanjala, mratibu wa miradi ya kitaifa UNIDO.

(Sauti ya Nanjala)

“Usambazaji wa ndizi ni wa juu lakini bei iko chini, shida kubwa ni kwamba mtu analazimika kuuza ndizi zake kwa bei ya chini na kama mkulima unajikuta unapata hasara, pili bila uboreshaji, ndizi nyingi zitakuwa sokoni na zitaanza kuoza lakini iwapo zinaboreshwa basi unaongeza muda wake wa matumizi.”

Ni kwa mantiki hiyo UNIDO inawawezesha wakulima katika eneo wanakokuza ndizi, ikiwemo kwa kuwajengea majengo ya kisasa ili kuimarisha uzalishaji wao na kukidhi viwango vya bidhaa zinazosafirishwa nje. Angel Mujurizi Salongo ni mnufaika wa mradi wa UNIDO na mwenyekiti wa kundi la wakulima la Rutunguru.

(Sauti ya Salongo)

“Tunapata ndizi aina ya bogoya na baada ya kuzipima tunaziweka kwenye hifadhi, tunaziweka kwa muda ili ziive baada ya kuiva, tunazimenya na kuzikatakata na baadaye tunaziweka ili zikauke.”

Matokeo yake ni ndizi zilizokaushwa ambazo wakulima wanajikusanya pamoja na kuziweka kwenye mifuko na kuuza ikiwemo nje ya nchi ambapo kwa mujibu wa Salongo wakulima wanatarajia kuimarisha juhudi zao kufuatia msaada wa UNIDO na hivyo kuimarisha vipato vyao.