Maendeleo yanayojali mazingira ni muhimu Afrika:Guterres

Ikiwa ni sehemu ya mradi wa 'kijani' wa UNDP, mafundi wakiweka mitambo ya nishati ya jua katika chuo cha polisi mjini Rajaf, Sudan Kusini 21 Agosti 2018
UNDP/Louis Fourmentin
Ikiwa ni sehemu ya mradi wa 'kijani' wa UNDP, mafundi wakiweka mitambo ya nishati ya jua katika chuo cha polisi mjini Rajaf, Sudan Kusini 21 Agosti 2018

Maendeleo yanayojali mazingira ni muhimu Afrika:Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa bara la Afrika kuhakikisha maendeleo yao yanakuwa safi na yanayojali mazingira.

 

Wito huo ambao ni sehemu ya ujumbe wake maalum kuhusu siku ya maendeleo ya viwanda Afrika inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 20, Antonio Guterres amesema , huu ni wakati muafaka kufanya hivyo wakati bara hilo likiingia katika utekelezaji wa kihistoria wa makubaliano ya biashara huria huku akiwachagiza kwamba ukuaji huo wa kiuchumi na maendeleo uwe wenye manufaa kwa watu wote  wa bara la afrika na sayari dunia.

Guterres amesisitiza kuwa, “maendeleo ya viwanda ni muhimu sana kwa uchumi endelevu na jumuishi kwa nchi za bara hilo la Afrika ambako sekta ya viwanda na uzalishaji inakuwa kwa kasi kuliko kiwango cha wastani cha dunia na utahitaji kusongezwa kwa kasi zaidi.”

Ukiwa umezinduliwa mwaka jana mkataba huo wa biashara huria barani Afrika AcFTA unatarajiwa kuleta katika soko angalau dola trilioni tatu na watumiaji zaidi ya bilioni moja.

Wakati huohuo Katibu Mkuu amesema sekta ya uzalishaji inatarajiwa kukuwa mara mbili zaidi ifikapo mwaka 2025 na kuunda mamilioni ya ajira.

“Natoa wito kwa nchi za Afrika kuchukua mtazamo thabiti wa sera za viwanda,  kutafuta, kupitia ushirika wenye nguvu wa wadau mbalimbali, mikakati ya viwanda safi, inayojali mazingira na ambayo inakuza fursa sawa za kiuchumi kwa kuzingatia uharaka wa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.”

Katibu Mkuu amehimiza umuhimu wa ahadi ya kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu barani Afrika, kwa Baraza Kuu kutangaza kwamba kipindi cha kuanzia 2016 -2025 kuwa ni muongo wa mapinduzi ya tatu ya viwanda kwa ajili ya Afrika.

Ameongeza kuwa na matokeo yake shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na maendeleo ya viwanda UNIDO  inaongeza msaada wa kiufundi kwa nchi za bara hilo.

Shirika hilo pia litashirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa katika miradi inayohusiana na masuala ya uhamishaji wa teknolojia, mnyororo wa thamani ya maendeleo ya biashara ya kilimo, nishati saditifu na maendeleo ya uchumi wa kanda maalum na viwanda.