Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNIDO, FAO na AU waibuka na mpango wa vijana kusongesha kilimo Afrika

Mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu  akishiriki mkutano wa lish bora Afrika kwenye TICADVII
©FAO/Life14
Mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu akishiriki mkutano wa lish bora Afrika kwenye TICADVII

UNIDO, FAO na AU waibuka na mpango wa vijana kusongesha kilimo Afrika

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkutano wa 7 wa Tokyo kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, TICADVII ukiendelea huko Yokohama nchini Japan, mashirika ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU pamoja na wadau wamezindua mpago wa kuchagiza ajira ya vijana kwenye sekta ya kilimo cha biashara barani humo. 

AU na mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la maendeleo ya viwada, UNIDO, chakula na kilimo FAO na wadau wamesema bara la Afrika ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya vijana duniani, ambapo zaidi ya milioni sita wako kwenye soko la ajira.

Ni kwa mantiki hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema “tunapozungumzia rasilimali watu tumainiwa barani Afrika tunamaanisha vijana na sekta ya kilimo cha biashara barani Afrika inatarajiwa kuwa na soko lenye thamani ya dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2030. Kwa hiyo kilimo kina fursa ambayo haijatumiwa vizuri ya kukabili changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.”

 Kwa kuzingatia hilo na ushirikiano wa nchi za kusini na ushirikiano wa utatu, mpango uliozinduliwa unalenga kuimarisha mifumo anuwai ya kibiashara kwa kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana Afrika.

Mpango utajikita katika kutoa usaidizi wa kiufundi, ujengaji uwezo na kubadilishana uzoefu miongoni mwa vijana wajasiriamali huku kipaumbele kikiwa ni kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Li Yong amesema ajenda 2063 ya Afrika inataka kuona Afrika yenye ustawi sawa kwa misingi ya ukuaji uchumi shirikishi na endelevu ukichochewa na ushiriki wa wanawake na vijana.

Hivyo amesema kujumuisha vijana kwenye sekta ya kilimo cha biashara ni kipaumbele kikuu cha utekelezaji wa mpango wa kina wa maendeleo ya sekta ya kilimo barani Afrika.