Kinachoendelea Hong Kong SAR kinatutia hofu:UN

13 Agosti 2019

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema anatiwa wasiwasi mkubwa na matukio yanayoendelea kwenye jimbo maalum la Hong Kong SAR na machafuko ambayo yameshika kasi katika siku za karibuni.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa ofisi ya haki za binadamu mjini Geneva Uswis, Kamishna Mkuu Michelle Bachelet “analaani aina yoyote ya machafuko au uharibifu wa mali na kumtaka kila mshiriki katika maandamano kutoa mawzo yao kwa njia ya amani.”

Kamishina huyo amesema anatambua dhamira ya mkuu mtendaji wa eneo hilo ya kutaka kushirikiana haraka iwezekanavyo na kusikiliza malalamiko ya watu wa Hong Kong.

Pia “ametoa wito kwa mamlaka na watu wa Hong Kong kushiriki katika majadiano ya wazi na jumuishi kwa lengo la kutatua changamoto zao kwa njia ya amani. Hii ndio njia pekee sahihi ya kufikia utulivu wa kisiasa wa muda mregfu na usalama wa umma kwa kuanzisha mifumo ya watu kushiriki katika masuala ya jamii na maamuzi yanayoathiri maisha yao.”

Kamishina mkuu amesisitiza kwamba uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, na haki ya kushiriki katika masuala ya jamii vinatambulika katika azimio la haki za binadamu na pia katika mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu za kisiasa na kiraia ambazo zimejumuishwa katika sharia za msingi za Hong Kong SAR.

Ofisi ya haki za binadamu imesema imetathimini ushahidi wa uvunjaji sharia unaofanywa na maafisa wa kutumia silaha nyepesi kwa njia ambazo zinapingwa na sharia za kimataifa , kwa mfano maafisa wa vikosi vya usalama wameonekana wakirusha mabomu ya kutoa machozi na mipira ya maji kwa umati wa waandamanaji au moja kwa moja kwa baadhi ya waandamanaji katika nyakati tofauti na kuweka mazingira ya hatari ya kifo au kujeruhiwa kwa waandamanaji hao.

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imeitaka mamlaka ya Hong Kong SAR kuchunguza matukio hayo mara moja na kuhakikisha vikosi vya ulinzi vinafuata sharia za kimataifa na ambapo inapolazimika ibadilishe sharia kwa maafisa hao katika kukabiliana na waandamanaji hasa pale ambapo sheria hizo hazizingatii viwango vya kimataifa.

Pia Kamishana mkuu ameitaka mamlaka ya Hong Kong SAR kujizuia na kuhakikisha kwamba haki za wale wanaoelezea mawazo yao kwa amani wanaheshimiwa na kulindwa huku ikihakikisha kwamba hatua zinazochukuliwa na maafisa wa ulinzi na usalama dhidi ya ghasia zozote ambazo zitajitokeza zitazingatia sheria na viwango vya kimataifa dhidi ya matumizi ya nguvu kupita kiasi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud