Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni rasmi, ofisi ya haki za binadamu ya UN kufunguliwa Sudan

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Asma Mohamed Abdalla wakitia saini makubaliano ya kuanzisha ofisi ya haki za binadamu ya UN nchini Sudan
UN News/Hafiz Kheir
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Asma Mohamed Abdalla wakitia saini makubaliano ya kuanzisha ofisi ya haki za binadamu ya UN nchini Sudan

Sasa ni rasmi, ofisi ya haki za binadamu ya UN kufunguliwa Sudan

Haki za binadamu

Hatimaye Sudan imetia saini makubaliano ya kufungua  ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwenye mji mkuu Khartoum na ofisi za mashinani kwenye majimbo ya Darfur, Blue Nile, Kordofan Kusini na Sudan Mashariki.

Makubaliano hayo yametiwa saini hii leo jijini New York, Marekani kati ya Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Asma Mohamed Abdalla, na kushuhudiwa na Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok ambao wako New York, kushiriki vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Geneva, Uswisi imemnukuu Bachelet akisema kuwa “tumeshuhudia kwa heshima kubwa azma ya wanawake wanaume na vijana nchini Sudan ya kuchagiza haki zao za kibinadamu,” huku akiongeza kwamba, “mwelekeo unaonekana kuwa na changamoto lakini tuko tayari kusaidia kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa wakati wa kipindi hiki cha mpito.”

Amesema kuwa kuwepo kwa mkataba huo wa kihistoria, ofisi yake ipo tayari kuambatana na Sudan kwenye safari muhimu ya kihistoria na kutoa msaada wowote unaotakiwa ili kufanikisha haki za binadamu hasa kwenye kipindi cha sasa cha mpito baada ya mageuzi.

Waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum

Ametaja maeneo manne ambayo watapatia msaada zaidi kufuatia majadiliano na serikali ya Sudan kuwa ni kutokomeza ukosefu wa usawa na kusaidia utungaji wa sheria za kujenga haki za kijamii na kiuchumi na kuwezesha ushiriki wa wanawake.

Pili, “kusaidia merekebisho  ya taasisi za sheria na kusaidia serikali kutunga sheria kwa mujibu wa wajibu wake kwa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuunda taasisi thabiti za kulinda haki za binadamu.”

Eneo la tatu kwa mujibu wa kamishna huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ni haki kwenye kipindi cha mpito hususan kusaidia uwajibikaji na maridhiano wakishirikisha ipasavyo manusura wa ghasia zilizotokea nchini humo.

Kuimarisha fursa za kidemokrasia ikiwemo ushiriki thabiti wa wanawake na makundi madogo ni eneo la nne akisema kuwa, “nyaraka ya kikatiba iliyotiwa saini tarehe 17 mwezi Agosti mwaka huu ina ahadi chanya kwa haki za binadamu. Natambua pia kuanzishwa kwa kamati huru ya kitaifa ya uchunguzi ili kuchunguza ukandamizaji wa waandamaji tarehe 3 mwezi Juni mwaka huu.”

Taarifa hiyo imetamatishwa kwa kumnukuu Bi. Bachelet akisema kuwa, “nasubiria kwa hamu kushirikiana na Sudan katika kujenga mazingira ya mafanikio yatokanayo na hatua za miezi michache iliyopita na kuhakikisha kuwa yanaweka msingi na hayarudishwi nyuma.”