Tuhakikishe watu ni msingi wa kila jambo tunalofanya 2019- Guterres

16 Januari 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaja maeneo matatu ya utekelezaji kwa mwaka huu wa 2019. 

Rambirambi kwa wananchi na serikali ya Kenya

Kabla ya kuanza hotuba yake hiyo, mbele ya wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York Marekani, Katibu Mkuu ametuma salamu zake za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Kenya kufuatia vifo vya watu 14 waliouawa kwenye shambulio la kigaidi jana huko Nairobi.

Ameelezea mshikamano na nchi hiyo akisema ugaidi katu haulalishwi kwa sababu yote.

Maeneo ya utekelezaji mwaka 2019

Kisha akaendelea na hotuba yake ya kurasa 9 ambapo Bwana Guterres ametaja maeneo ya kuchukua hatua zaidi kuwa ni kukabili mabadiliko ya tabianchi, kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, na kutumia teknolojia mpya kuchagiza vipaumbele hivyo iwe kwenye elimu au afya na kuhakikisha teknolojia haziengui wengine kwenye ajira.

Hata hivyo amesema wakati  huu ambapo maadili yanakumbwa na changamoto..

“Tunahitaji kampeni mpya kuhusu maadili ya haki za binadamu na utu wa binadamu,  vitu ambavyo tunavithamini. Ni lazima viwe na uhalisia kwa kila mtu.”

Watu ni msingi wa kila kitu

Na msingi ni Katiba iliyoanzisha Umoja wa Mataifa kwasababu,  "kwa maadili ambayo tunatetea yawepo, tunahitaji kuonyesha kuwa tunaelewa shaka na shuku za watu. Tunahitaji kushughulikia mzizi wa kile kinachosababisha watu kuona wanapuuzwa kwenye jamii  yetu  hii ambayo inasonga kwa kasi kubwa.”

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema, "hebu na tuendelee kudhihirisha thamani yetu kwa kuchagiza juhudi zetu za kuendeleza dunia yetu kwa kutomuacha mtu yeyote nyuma.”

Akiangazia mwaka uliopita ameshukuru nchi wanachama kwa mafanikio yaliyochagizwa na ushirikiano wa kimataifa ikiwemo makubaliano ya amani Sudan Kusini sambamba na mikataba ya kimataifa ya wahamiaji na wakimbizi.

Umoja wa Mataifa  nao unajibadili uwe na thamani kwa watu

Katibu Mkuu hata hivyo amegeukia Umoja wa Mataifa chombo ambacho anaongoza akisema kuwa na chenyewe kinakabiliwa na ukosefu wa imani miongoni mwa wale ambao unapaswa kuwaongoza. Kwa kuzingatia hali hiyo amesema tayari chombo hicho kimeanza kufanya marekebisho makubwa kuhakikisha kuwa kinadhihirisha thamani yake kwa binadamu.

Miongoni mwa marekebisho ni  mfumo mpya wa maendeleo ili kuhakikisha yanaleta mabadiliko kwa wananchi mashinani, mfumo thabiti wa zaidi wa amani na usalama pamoja na mfumo bora wa usimamizi ili Umoja wa Mataifa uwe na tija ambapo amesema , "sote tunataka shirika lenye  kasi zaidi, fanisi, linaloenda na mazingira. Ndio maana tunajifanyia marekebisho makubwa - kuhudumia watu vizuri zaidi."

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter