Espinosa ataja vipaumbele vyake mkutano 73 ukibakiza miezi 8

15 Januari 2019

Ikiwa imesalia miezi nane kabla ya kumalizika kwa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hii leo Rais wa baraza hilo, Maria Fernanda Espinosa amezungumza na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kueleza vipaumbele saba atakavyozingatia wakati wa kipindi hicho.

Akihutubia katika kikao kisicho rasmi cha baraza hilo jijini New York, Marekani hii leo, Bi. Espinosa amesema vipaumbele hivyo vinaendana na maudhui makuu ya mkutano wa 73 wa Baraza Kuu ambayo ni kufanya Umoja wa Mataifa uwe na maslahi kwa watu wote:uongozi na uwajibikaji wa pamoja kwa jamii yenye amani, usawa na endelevu.

Pamoja na kutambua mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ya mkutano huo wa 73 ikiwemo kupitisha maazimio na maamuzi, Bi. Espinosa ametaja vipaumbele kuwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wakati huu ambapo amesema unakabiliwa na tishio kubwa akisema katika kusongesha ushirikiano huo tarehe 4 mwezi ujao ataitisha mkutano na marais wastaafu wa Baraza Kuu la umoja wa mataifa kuona jinsi gani Umoja wa Mataifa unaweza kuimarisha ushiririkiano wa kimataifa.

Kipaumbele cha pili ni utekelezaji wa mikataba ya mipya ya kimataifa ikiwemo ule wa wahamiaji na wakimbizi ambayo ilipitishwa mwishoni mwa mwaka jana.

Bi. Espinosa ametaja vipaumbele vingine kuwa ni usawa kijinsia, ambapo ataitisha kikao cha ngazi ya juu kuhusu wanawake kwenye  uongozi kando mwa mkutano wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani tarehe 12 mwezi Machi mwaka huu.

Wakati huu ambapo suala la ajira zisizo na hadhi linapigiwa chepuo ili lipatiwe suluhu, Rais huyo amepatia kipaumbele cha nne suala hilo akisema “tunahitaji kuwaweka watu kama kitovu cha maendeleo na kuchechemua haki za jamii zilizo pembezoni.”

Vipaumbele vingine ni uhifadhi wa mazingira, haki za watu wenye ulemavu, na amani na usalama.

Amekumbusha nchi wanachama kuwa sambamba na vipaumbele hivyo ni umuhimu wa kuelimisha jamii kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs akisema uelewa wake ndio jawabu la kuwezesha yafanikiwe.

Kwa mantiki hiyo amekumbusha wajumbe kuhusu kikao cha ngazi ya juu cha kisiasa kuhusu maendeleo endelevu ambacho kitafanyika mwezi Septemba mwaka huu wa 2019 wakati wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 

TAGS: Maria Fernanda Espinosa, UNGA73

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud