Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lajčák akabidhi kijiti cha kuongoza Baraza Kuu Maria Espinosa

Miroslav Lajčák,Rais wa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu akikabidhi rungu la kuongoza kikao kwa rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu María Fernanda Espinosa kwenye makao makuu ya UN New York, Marekani hii leo.
UN /Manuel Elias
Miroslav Lajčák,Rais wa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu akikabidhi rungu la kuongoza kikao kwa rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu María Fernanda Espinosa kwenye makao makuu ya UN New York, Marekani hii leo.

Lajčák akabidhi kijiti cha kuongoza Baraza Kuu Maria Espinosa

Masuala ya UM

Mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umetamatishwa hii leo ambapo aliyekuwa rais wake Miroslav Lajčák ametaja mambo sita  muhimu aliyobaini wakati wa uongozi wake tangu mwezi Septemba mwaka jana.

Akihutubia kikao cha mwisho cha mkutano huo hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York nchini Marekani, Bw. Lajčák ametaja masuala sita akisema  Kwanza ni mwelekeo wa amani. Kuhusu hili mkataba wa Umoja wa mataifa ni madhubuti kuhusu hilo. Unatutaka kuokoa  kizazi kijacho dhidi ya  makali ya vita.Lakini hatukuweza kufanikisha azma hii. Kipindi kilichopita tumekuwa tu kama wafufuaji. Tumekuwa na walinda amani na wapatanishi wazuri , tatizo ni kuwa hufika wakiwa wamechelewa.”

Ameyataja mengine kama vile  umuhimu wa kutunza sayari ya dunia katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi, akisema kutokana na umuhimu wake suala hilo limekuwa likitajwa kila mara katika vikao.

Pia ametaja suala la mazungumzo kama jambo muhimu ijapokuwa wakati huu amesema linaonekana kama limepewa kisogo.

Miroslav Lajčák, Rais wa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la UN akihutubia kikao cha 116 na cha mwisho leo tarehe 17 Septemba 2018
UN /Manuel Elias
Miroslav Lajčák, Rais wa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la UN akihutubia kikao cha 116 na cha mwisho leo tarehe 17 Septemba 2018

Kuhusu suala la mageuzi ndani mwa Umoja wa Mataifa Bwana Lajčák amesema haliepukiki ili chombo hicho chenye wanachama 193 kiweze kwenda sambamba na  mazingira yanayobadilika kila mara..

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye pia amehudhuria kikao hicho akatumia fursa hiyo kutoa tathmini yake ya mkutano wa 72 akisema  “Mkutano wa 72 ulikuwa na shughuli nyingi na pia ulikuwa hai hasa kushughulikia masuala kuanzia mabadiliko ya tabianchi, upokonyaji wa silaha na  maendeleo ya kiuchumi. Mlidhihirisha mchango wa maana wa Baraza Kuu kwa kushughulikia masuala yanayowagusa watu duniani pamoja na matarajio yao. Pia mkutano ulifanya juhudi mbalimbali za mataifa wanachama za   kuimarisha Umoja wa Mataifa.”

Halikadhalika Bwana Guterres amempongeza Bw. Lajčák kwa uongozi wake mzuri wa mkutano huo.

Baada  ya hotuba itifaki ilizingatiwa na Bw. Lajčák ambaye alianza kuongoza chombo hicho mwezi Septemba mwaka jana, akakabidhi rungu la  urais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa Maria Fernanda Espinosa.