Wakimbizi 20,000 kutoka Afghanistani wahamia Canada tangu mwaka jana- IOM

23 Septemba 2022

Suala la kuhamishia wakimbizi nchi ya tatu kama njia mojawapo ya kutekeleza mkataba wa kimataifa wa wakimbizi linaendelea kuzaa matunda ambapo shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa linasema tangu mwezi Agosti mwaka jana wa 2021 hadi leo hii limesaidia wakimbizi 20,000 kutoka Afghanistan kuhamia nchini Canada.

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema idadi hiyo imefikia baada ya kuwasili mjini Toronto, Canada kwa ndege kutoka Falme za kiarabu ikiwa na watu 337, miongoni mwao ni watoto 121 wakiwa wameambatana na maafisa wa IOM.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, António Vitorino amesema, “jukumu la kuhamishia wakimbizi nchi ya tatu kwa njia salama na yenye utu, limekuwa la IOM kwa zaidi ya miaka 70.”

Amesema wanaendelea kushirikiana na serikali ya Canada na nchi nyingine kuhakikisha makumi ya maelfu ya waafghanistan walio hatarini wanapatiwa fursa ya kuanza upya maisha yao katika mazingira salama na yenye usaidizi.

IOM inasema ubia wake wa muda mrefu na serikali ya Canada imewezesha siku za awali kuhamishia nchini humo raia wa Syria na Ira, na kwamba “shirika hilo litaendelea kushirikiana na wadau wengine duniani kusaidia azma ya Canada ya kukubali angalau wakimbizi 40,000 kutoka Afghanistan.”

Pamoja na kuratibu ndege za kusafirisha wakimbizi hao, IOM inasaidia wakimbizi hao na mchakato wa maombi, na kupatia tathmini za uchunguzi wa kiafya kabla ya safari sambamba na kuwaandaa na mafunzo ya jinsi ya kuishi Canada.

Kwa kushirikiana na jamii za usaidizi wa kibinadamu duniani, IOM pia inasaidia wakimbizi wa ndani nchini AFghanistani hasa makabila madogo, na makundi mengine yaliyo pembezoni kama vile watu wenye  ulemavu, wanawake ,wasichana na LGBTIQ.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter