Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaitisha mkutano na wadau kuijadili suluhu ya Venezuela

Familia ya wakimbizi wa Venezuela wakivuka daraja baina ya Ecuador na Colombia  4 June 2019
© UNHCR/Santiago Escobar-Jarami
Familia ya wakimbizi wa Venezuela wakivuka daraja baina ya Ecuador na Colombia 4 June 2019

UNHCR yaitisha mkutano na wadau kuijadili suluhu ya Venezuela

Amani na Usalama

Venezuela, moja kati ya Mataifa ambayo wananchi wake wanalikimbia kwa wingi takwimu kwenda kuomba hifadhi mataifa mengine ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha takribani robo ya wananchi wake wamekimbia hali ambayo imeshafanya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa kuitisha mkutano hii leo kutafuta suluhu ya kudumu. Tuungane na Leah Mushi kwa undani wa taarifa hii

Jamuhuri ya Venezuela ni taifa lenye watu milioni 28 lakini kila uchao wananchi wake wanamiminika katika mipaka ya nchi jirani kuomba hifadhi. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR  takwimu za mpaka sasa zinaonesha Wavenezuela milioni 5.6 wameikimbia nchi yao, sababu kubwa ni mizozo inayoendelea ndani ya taifa hilo. 

Wengi wa wakimbizi hawa wanakimbilia Colombia ambako abisha hodi  katika Kituo cha afya, Franyimar binti wa miaka 5 anafanyiwa uchunguzi wa ulemavu wa mguu wake mmoja hali inayosababisha kushindwa kutembea vizuri. 

Huyu ni mmoja kati ya wa watoto 4 wa Veronica, mama ambaye anasema sababu kubwa ya kukimbia Venezuela ni kutafuta matibabu ya binti yake, na sasa amepata dawa kwa ajili ya kumtibu.

Colombia inaongoza kuwa na wakimbizi wengi wa Venezuela, mwezi February mwaka huu wa 2021 walianzisha mpango maalum wa kutoa vibali vya kuishi kwa miaka 10 na Wavenezuela milioni 1.7 wameshanufaika akiwemo Sikiu, ambaye sasa amepata matumaini kuwa mwanae Lucas atapata mahitaji yote muhimu.

Wahamiaji wa Venezuela nchini Colombia. Takriban watu 5000 wamekuwa wakivuka mpaka kila siku kutoka Venezuela kwa mwaka mmoja uliopita zimesema takwimu za UN.Colombia Aprili 2019
©UNHCR/Vincent Tremeau
Wahamiaji wa Venezuela nchini Colombia. Takriban watu 5000 wamekuwa wakivuka mpaka kila siku kutoka Venezuela kwa mwaka mmoja uliopita zimesema takwimu za UN.Colombia Aprili 2019

Nikitoka Colombia nashuka chini zaidi, nafika katika nchi ya Peru ambapo hapa anaonekana Dkt Carmen Parra, akiwa anamaliza zamu yake ya saa 24 katika kituo cha kusaidia wagonjwa wanaougua Corona.

 Haikuwa rahisi kwa Daktari Carmen mkimbizi wa Venezuela kupata kazi, alipofika hapa alihangaika kwa miaka miwli kufanya kazi na kuwa mhudumu mgahawani, mkaribisha wageni ofisini kabla ya UNHCR na asasi ya kiraia kumsaidia kuvithibitisha vyeti vyake vya udaktari nchini Peru.

Sofia Brito binti wa miaka 12 alitembea kutoka Venezuela mpaka hapa Peru  akiwa yeye na mama yake na wadogo zake wa kiume. Sasa ndoto zake zote zimezimwa kwa kukaa nyumbani kuwalea wadogo zake wakati mama yake akisaka ajira ili awaletee chakula na mavazi.

Simulizi za visa hivi zimejaa nchi jirani za Chile, Brazil, Ecuador mpaka Mexico na kote wakimbizi wanawasili wengine wakiwa katika hali mbaya wakikosa hata nguo za kuwasaidia kujikinga na baridi kali usiku.

Hali hii ni dhahiri haina afya si kwa wananchi wa Venezuela pekee bali dunia kwa ujumla na inatakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka, ndio maana UNHCR pamoja na serikali ya Canada, katika kutafuta suluhu ya kudumu hii leo wanaendesha mkutano na wadau mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara na makampuni binafsi kuona namna ya kuisaidia Venezuela.