Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamlaka DRC rejesheni huduma ya intaneti

Wapiga kura wakiangalia majina yao kwenye orodha ya wapiga kura wakati wa uchaguzi wa rais na wabunge huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC tarehe 30 Desemba 2018
MONUSCO/Alain Likota
Wapiga kura wakiangalia majina yao kwenye orodha ya wapiga kura wakati wa uchaguzi wa rais na wabunge huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC tarehe 30 Desemba 2018

Mamlaka DRC rejesheni huduma ya intaneti

Haki za binadamu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu  haki ya binadamu ya uhuru wa kujieleza, David Kaye, ameisihi serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC irejeshe huduma ya intaneti nchini humo.

Huduma hiyo ilikatwa siku moja baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo tarehe 30 mwezi uliopita.

Bwana Kaye, kupitia taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, amesema “ukataji wa jumla wa mtandao wa intaneti ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na hauwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile.”

Amesema kupata taarifa ni muhimu katika kuhalalisha mchakato mzima wa uchaguzi na kwamba kukatwa kwa huduma ya intaneti siyo tu kunakwamisha uwezo wa watu kupata taarifa bali pia haki yao ya kupata huduma za msingi.

Maafisa waandamizi wa serikali ya DRC wamenukuliwa wakisema kuwa hatua hiyo ya kukata huduma ya intaneti na ujumbe mfupi, SMS,  ililenga kurejesha utulivu miongoni mwa wananchi baada ya matokeo bandia uchaguzi kuanza kusambazwa na kwamba “kukatwa kwa huduma hizo kutaendelea hadi kutakapochapishwa kwa matokeo rasmi.”

David Kaye, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki za kujieleza na kutoa maoni wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New Yrok, Marekani tarehe 25 Oktoba 2018
UN /Rick Bajornas
David Kaye, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki za kujieleza na kutoa maoni wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New Yrok, Marekani tarehe 25 Oktoba 2018

Hata hivyo ripoti zinaonyesha kuwa kutokuwepo kwa huduma hiyo ya intaneti kunakwamisha harakati za waangalizi wa uchaguzi na mashuhuda ambao wanategemea taarifa kutoka vituo vya kupiga kura vilivyoko vijijini.

Halikadhalika inakwamisha uwezo wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO kuwasiilana na wadau wake mashinani ikiwemo wale wanaohusika na huduma za ulinzi.

Ni kwa mantiki hiyo Bwana Kaye amesihi mamlaka za DRC zirejeshe huduma hizo kwa kutambua kuwa ni jambo la dharura na kuzingatia umuhimu wa mchakato wa uchaguzi.

Mwaka 2016, Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio ambalo linalaani hatua zozote zenye nia ya kuzuia au kuvuruga usambazaji wa taarifa mtandaoni likisema ni ukiukwaji wa haki za binadamu za kimataifa na kutaka serikali zijizuie kuchukua hatua kama hizo.

Hatua hiyo ilifuatiwa na azimio la pamoja la mwaka 2015 la wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wa kikanda k uhusu haki za kujieleza ambalo lilieleza kuwa kufungwa kwa mitandao ya intaneti hakuwezi kuhalalishwa chini ya sheria za haki za binadamu.

Bwana Kaye amesema ataendelea kufuatilia hali ilivyo DRC na yuko tayari kushauriana na mamlaka iwapo msaada wake utahitajika.