Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mboji yabadili maisha kwa wakulima Bangladesh

Taka zinazochanganywa na kinyesi cha ng'ombe huwezesha wakulima kupata mboji ambayo ni kirutubisho cha udongo na mazao.
UNDP/Vietnam
Taka zinazochanganywa na kinyesi cha ng'ombe huwezesha wakulima kupata mboji ambayo ni kirutubisho cha udongo na mazao.

Mboji yabadili maisha kwa wakulima Bangladesh

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Bangladesh, ziara zilizoandaliwa na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kwa ajili ya wakulima katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, zimebadilisha mbinu za kilimo na hatimaye kuongeza tija. 

Nchini Bangladesh, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanaishi vijijini na wengi wao ni wakulima, mashamba  yao yakiwa ni madogo ambapo kwa wastani shamba si zaidi ya heka moja.

Mazingira haya yanamanisha kuwa ni vigumu kwa mkulima mmoja mmoja kuweza kunufaika na kilimo kwa kuwa gharama za pembejeo ikiwemo mbolea ni za juu na hata akivuna hawezi kushindana kwenye soko.

FAO ilichagiza wakulima kujiunga kwenye vikundi na kuwapeleka kwenye ziara za mafunzo Kenya, India na Ufilipino ambako pamoja na mambo mengine wakulima walijifunza kutengenza mboji, yaani mbolea itokanayo na kinyesi cha ng’ombe ikichanganywa na mimea, mbolea ambayo wanatumia kwenye mashamba na pia kuuza.

Abdul Jabbar, kiongozi wa kikundi hicho anasema awali walikuwa sawa na chura kwenye pango lakini sasa wameelimika..

“Mboji inalenga uhai kwenye udongo, wakulima wengi wamebaini faida na mahitaji yanaongezeka kila siku. Kwanza tunasambaza kinyesi cha ng’ombe kwenye eneo tunalotaka kutengeneza mboji. Kisha tunaongeza minyoo na tunaacha kwa siku 15, tunageuzageuza na baada ya siku 20 mboji iko tayari kwa kutumia au kuuza.”  

Kila mwezi mkulima Jabar anageuza kinyesi cha  ng’ombe na kupata tani 5 za mboji ambayo ni mbolea isiyoharibu ardhi na mimea na anafundishwa wakulima wengine 44 kwenye mtandao wa wakulima Bangladesh ili hatimaye waweze kuuza na kujipatia kipato.