Skip to main content

Bangladesh hakikisheni mnafanya uchaguzi huru na wa haki: UN

Uchaguzi wa huru na haki utakuwa na maana kubwa kwa mstakabali wa watu wa Bangladesh kama kijana huyu ambaye pia ni dereva wa Lori
World Bank/Scott Wallace
Uchaguzi wa huru na haki utakuwa na maana kubwa kwa mstakabali wa watu wa Bangladesh kama kijana huyu ambaye pia ni dereva wa Lori

Bangladesh hakikisheni mnafanya uchaguzi huru na wa haki: UN

Amani na Usalama

Kuelekea uchaguzi mkuu nchini Bangladesh unaotarajiwa kufanyika jumapili hii ya tarehe 30 mwezi huu wa Desemba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa hii leo mjini New York Marekani na msemaji wake, amewasihi wadau wote Bangladesh wahakikishe wanaweka mazingira yasiyo na vurugu, vitisho wala kulazimishwa, kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ili kuwezesha uchaguzi wa amani, halali na unaohusisha watu wote.

“Raia wote wa Bangladesh, wakiwemo jamii za watu wachache na pia wanawake, wanatakiwa kujihisi salama na hakika katika kutimiza haki ya kupiga kura. Mashirika ya kiraia na waangalizi wa uchaguzi wanatakiwa kupewa nafasi ya kutosha kutimiza jukumu lao katika mchakato mzima wa uchaguzi” sehemu ya taarifa ya Guterres imeeleza.

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbushia ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kuisaidia Bangladesh yenye amani na demokrasia.

Hivi karibuni kuelekea mwishoni mwa kampeni za uchaguzi kumekuwa na mvutano mkali kati ya wale wanaoumuunga mkono Sheikh Hasina Wazed Waziri Mkuu wa sasa wa Bangaldesh na wale wanaompinga.

Bi Hasina ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Bangladesh, Sheikh Mujibur Rahman amekuwa madarakani tangu mwaka 2009 akitajwa kuwa ndiye Waziri Mkuu ambaye amedumu katika madaraka hayo kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine yeyote katika historia ya nchi hiyo. 

Mpinzani wa karibu wa Hasina ni Khaleda Zia mwanamke mwenye umri wa miaka 73 ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu katika vip[indoi viwili. Hata hivyo Zia wa Bangladesh Nationalist Party (BNP) hivi sasa yuko jela kutokana na tuhuma za rushwa ambazo anazikanusha akidai kuewa zina uhusiano na siasa. Hivi sasa chama chake kinaongozwa na Kamal Hossain mwanasheria msomi wa Chuo Kikuu cha Oxford na waziri wa zamani wa sheria.

Vyombo mbalimbali duniani vimeonekana kupokea maoni na maswali ya watu kutoka kote duniani na swali kubwa likiwa kwa kuwa mpinzani mkuu wa Waziri Mkuu aliyeko madarakani amezuiliwa kugombea na yuko jela, ni nani atakuwa waziri mkuu wa Bangladesh ikiwa muungano wa upinzani utashinda?

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.