Bustani zinazoelea Bangladesh zaleta nuru kwa wakulima wanaokumbwa na mafuriko

4 Disemba 2018

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linasema kulingana na mwelekeo wa sasa wa tabianchi, harakati zozote za kilimo ni lazima zizingatie kilimo ambacho kinahifadhi mazingira.

Kupitia chapicho kwenye wavuti wake, FAO inasema hatua hizo ni muhimu kwa sababu kilimo ni miongoni mwa sekta ambazo zinaongoza duniani kwa kutoa hewa chafuzi zinazosababisha ongezeko la joto.

Hata hivyo FAO inasema iwapo hatua sahihi zitachukuliwa, kilimo kinaweza kuwa mkombozi dhidi ya mabadilko ya tabianchi kwa kusaidia jamii kuhimili athari za mabadiliko hayo na wakati  huo huo kuhifadhi udongo wenye rutuba.

FAO inaenda mbali inasema kuwa zaidi ya robo tatu ya wakazi masikini duniani wanaishi vijijini na tegemeo lao kubwa ni kilimo ili kujiongezea kipato na hivyo basi mabadiliko ya tabiachi bila hatua sahihi yatazidisha machungu ambayo tayari jamii hizo zinakabiliana nayo.

Ni kwa mantiki hiyo FAO imeanzisha miradi ya kilimo kinachokabili tabianchi, CSA ambacho kinahakikisha mifumo ya kilimo inasaidia wakulima kuwa na uhakika wa chakula na wakati huohuo kujipatia kipato licha ya mabadiliko ya tabianchi.

KILIMO KINACHOJALI MAZINGIRA UKANDA WA SAHEL

FAO inasema tayari kilimo cha aina hiyo kimeanza kuzaa matunda, ikitolea mfano wakulima nchini Niger na Burkina Faso kwenye ukanda wa Sahel ambako kwa msaada wa shirika hilo na Muungano wa Afrika, AU wanarejesha hali ya rutuba kwenye maeneo kame.

“Kwenye eneo hilo ambako ukataji miti ulitishia kuwepo kwa jangwa, ardhi inatengwa na kuwekewa uzio ambapo mbegu zilipandwa kwenye eneo la heka 12,000 na wananchi kuhamasishwa na kujengewa uwezo wa kuuza bidhaa zisizo za mbao ili waondokane na utegemezi kwenye biashara moja pekee,” imesema FAO.

BUSTANI ZINAZOELEA BANGLADESH

Mfano mwingine ni bustani zinazoelea nchini Bangladesha ambako mvua kubwa za mara kwa mara pamoja an vimbunga na ongezeko la kina cha maji ya bahari vimesababisha mafuriko. “Hali hii husababisha maji kutwama, mazao kuoza na eneo la ardhi ya kilimo linakuwa ni dogo,” imefafanua FAO.

FAO kwa kushirikiana na wakulima wenyewe walio na stadi za kijadi, walibadili eneo ambalo hutwama maji kila mwaka kuwa bustani zinazoelea.

Shirika hilo limesema “vipande vya shamba vinavyoelea kwenye maji hupandwa mboga. Wakati wa mwezi Juni na Julai huandaa vitalu hivyo vyenye umbo la mstatili ambako hupanda aina 30 ya mboga kama vile bamia, matango, kabichi, nyanya na pilipili.”

FAO inasema matokeo ya mifumo hii ya kilimo yamejenga uelewa mzuri zaidi wa aina za vichocheo na vikwazo vya kutumia mbinu hii ya kilimo na pia kuwapatia wakulima fursa ya kukabiliana na vikwazo hivyo na hatimaye kujiongeza kiuchumi na kutokomeza njaa.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter