UNHCR yaruhusiwa kukutana na msichana aliyezuiliwa katika uwanja wa ndege Bangkok.

7 Januari 2019

Mamlaka za Thailand zimeliruhusu shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR kumfikia Rahaf Mohammed Al-qunun mwenye umri wa miaka 18 raia wa Saudia katika uwanja wa ndege wa Bangkok kutokana na mahitaji yake ya ulinzi wa kimataifa, taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNICEF iliyochapishwa katika wavuti wa shirika hilo imeeleza.

UNHCR imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu maendeleo ya kuzuiliwa kwa Rahaf katika uwanja huo wa ndege.

Taarifa hiyo imesema Rahaf aliyaambia makundi ya watetezi wa haki za binadamu pamoja na vyombo vya habari kuwa alizuiliwa katika uwanja wa ndege wa Bangkok alipokuwa akipita kutokea Kuwait na akanyang’anywa hati yake ya kusafiria.  Rahaf aliikimbia familia yake akihofia Maisha yake na alikuwa anajaribu kukimbilia nchini Australia ambako alikuwa na matumaini ya kuomba hifadhi.

Mara kwa mara UNHCR imekuwa ikitetea kuwa wakimbizi na watafuta hifadhi, baada ya kuthibitishwa kuwa wana uhitaji wa kulindwa kimataifa hawawezi kurejeshwa katika nchi zao kwa mujibu wa kanuni inayozitaka nchi kutowafukuza au kuwarejesha watu kwenye himaya ambako Maisha au uhuru wao unaweza kutishwa.

Kanuni hii inatambuliwa kuwa ni sheria ya ya kimataifa, na pia inatambulika nchini Thailand.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali duniani, msichana huyu amekuwa akinyanyaswa na familia yake huko nchini Saudia Arabia na alifanikiwa kuikimbia familia hiyo wakiwa mapumzikoni nchini Kuwait.

Ameeleza kuwa familia yake ingemrudisha nchini mwake ambako amekuwa akipigwa na kunyanyaswa sana maisha yake yote ikiwemo kufungiwa katika chumba, kupigwa na kaka yake na hata hakuwa na maamuzi kuhusu nywele zake kwani kuna kipindi walimfunga ndani ya chumba kwa miezi sita kwa kuwa tu alinyoa nywele katika mtindo ambao hawakuuependa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud