Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ilivyo Myanmar ni mapema mno warohingya kurejea - Mtaalamu

© UNHCR / Andrew McConnell
Watoto waRohingya katika kambi ya Chonkhola huko Chakdhala, Bangladesh.

Hali ilivyo Myanmar ni mapema mno warohingya kurejea - Mtaalamu

Haki za binadamu

Mfumo unaotumiwa na mamlaka nchini Myanmar kukandamiza makabila madogo ikiwemo waislamu wa Rohingya ni wa kusikitisha.

Amesema Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Yanghee Lee, huko Seoul nchini Korea Kusini hii leo akisisitiza kuwa kwa kuzingatia hali hiyo ni mapema mno kuzungumzia kuwarejesha makwao warohingya.

Akizungumza baada ya ziara zake huko Thailand na Bangladesh mwezi uliopita kusaka ukweli wa ukiukwaji wa haki Myanmar baada ya serikali hiyo kumzuia kuingia nchini humo Bi. Lee amesema..

(Sauti ya Bi. Yanghee Lee)

“Kile ambacho serikali ya Myanmar inadai inafanya operesheni za kijeshi au usalama ni mfumo ulioandaliwa wa ukandamizaji, ghasia na ukiukwaji wa haki dhidi ya makabila. Wakati ripoti kutoka jimbo la Rakhine zimeibua kauli kali kutoka jamii ya kimataifa, kwa wengi nchini Myanmar hali hiyo ni mambo ya kutisha ambayo wamezoa kuyashuhudia.”

Amesema pamoja na ukatili, serikali ya Myanmar pia inabinya fursa ya demokrasia ambapo hata serikali ya sasa ya kiraia iemshindwa kufungua zama mpya za uwazi na badala yake inaendeleza vitendo vya ukandamizaji kama zama zilizopita.

Bi. Lee, ametaka serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia kuondokana na mifumo kandamizi iliyopita na badala yake iruhusu watu ambao wamekimbia nchi hiyo warejee ambako ndiko makazi yao.

(Sauti ya Bi. Yanghee Lee)

 “Bila usawa, Myanmar katu haitakuwa huru dhidi ya ghasia na vitendo katili vilivyozoeleka vitaendelea. Mzunguko wa ghasia lazima uishe na Myanmar lazima iungwe mkono katika kutekeleza marekebisho ya kimfumo thabiti na dhati ambayo yanahitajika haraka.”