Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangladesh wawajibisheni wanaokiuka haki za binadamu kutokana na siasa.

Wakazi wa mitaa isiyopangwa katika mji kuu wa Bangladesh, Dhaka.
World Bank/Dominic Chavez
Wakazi wa mitaa isiyopangwa katika mji kuu wa Bangladesh, Dhaka.

Bangladesh wawajibisheni wanaokiuka haki za binadamu kutokana na siasa.

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Ravina Shamdasani mjini Geneva, Uswisi imesema inaguswa na vurugu na kile kinachosemwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Bangladesh kabla, wakati na baada ya uchaguzi uliofanyika tarehe 30 mwezi uliopita wa Desemba.

Bi. Shamdasani amesema kuna ripoti za uhakika kuhusu vifo na majeruhi wakati wa uchaguzi na kwamba, “kuna dalili zinazoleta wasiwasi kuwa mateso yanaendelea kufanywa, hasa dhidi ya wapinzani wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kimwili na uovu, kukamatwa kiholela, unyanyasaji, kutoweka na kufunguliwa kesi za uhalifu.”

Aidha amesema kuna taarifa za kusikitisha kuwa wanahabari wananyanyaswa, kujeruhiwa na pia vifaa vya kuharibiwa pamoja na masuala mengine ambayo yanazuia taarifa huru kuhusu uchaguzi.

“Takribani wanahabari wawili wamekamatwa kwa kutumia sheria ya usalama wa mitandao kutokana na ripoti zao walizozitoa kuhusu uchaguzi. Vituo vya habari vipatavyo 54 na tovuti nyingine vimefungwa tangu Desemba 10 na pia vikwazo vingi kuhusu intaneti vimekwamisha uhuru wa kijueleza,” Bi. Shamdasani amesisitiza.

Ameeleza pia kuwa wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika, wanachama wa vyama vya upinzani na wananchi ambao wamekuwa wakiuzungumzia uchaguzi wanakamatwa.

“Tunazisihi mamlaka kufanya uchunguzi wa haraka, ulio huru, usio na upendeleo na pia wenye ufanisi kuchunguza vitendo vyote vya kidhalimu na ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanyika kuhusiana naa uchaguzi kwa lengo la kuwawajibisha wale wanaohusika bila kujali uhusiano wao wa kisiasa” Bi Shamdasani ametamatisha.