Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko mapya yazuka Myanmar, OHCHR yatoa wito raia walindwe

Makazi ya wakazi wa kata ya Aung Mingalar mji wa Sittwe, jimbo la Rakhine, Myanmar.
OCHA/P.Peron
Makazi ya wakazi wa kata ya Aung Mingalar mji wa Sittwe, jimbo la Rakhine, Myanmar.

Machafuko mapya yazuka Myanmar, OHCHR yatoa wito raia walindwe

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu imeelezea kusikitishwa na ongezeko la machafuko katika jimbo la Rakhine katika wiki za hivi majuzi na imelaani mashambulizi ya kulenga yanayolelekezwa kwa raiai na vikosi vya usalama vya Myanmaar na wapiganaji waliojihami katika muktadha wa mapigano yanayoendeshwa na jeshi la Rakhine kwa jina Arakan.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa Ofisi ya haki za binadamu, Ravina Shamdasani amesema mzozo kati ya jeshi la Myanmar lijulikanalo kama Tatmadaw na jeshi la Arakan umesababisha ongezeko la mauaji ya raia, nyumba kuteketezwa, kukamatwa kiholela, kutekwa, kuchomwa moto maeneo ya raia na uharibifu wa mali za kitamaduni.

Bi. Shamdasani ameongeza kwamba machafuko yameathiri raia wa makabila tofauti katika majimbo ya Rakhine na Chin ikiwemo wa Rakhine, Rohingya, Chin, Mro na Daignet. 

Aidha, “kwa mujibu wa ripoti tulizozipokea mapigano yameongezeka katika miji ya Buthidaung, Rathedaung, Kyauktaw, Mrauk-U, and Sittwe jimbo la Rakhine katika kipindi cha wiki chache zilizopita na kupelekea watu 20,000 kufurushwa makwao. Halikadhalika hali ni mbaya zaidi kwa kuwa serikali imesitisha upelekaji misaada ya kibinadamu tangu mwezi Januari mwaka huu.”

Akitolea mfano mashambulizi ya jumatano wiki hii, Bi. Shamdasani amesema helikopta za wanajeshi zilipaa kwenye kijiji cha Hpon Nyo Leik kusini mwa mji wa Buthidaung na kufyatulia risasi raia waliokuwa wanachunga ng’ombe na kuwaua takriban watu saba na kuwaacha watu wengine 18 na majeraha, akisema ni kwa mujibu wa taarifa kutoka mashinani.

Kwa kuzingatia hali ya sasa ofisi ya haki za binadamu imetoa wito kwa wanajeshi wa Tatmadaw na Arakan kusitisha uhasama na kuhakikisha ulinzi wa raia. Aidha ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu uruhusiwe ikiwemo katika maeneo yaliyoathirika kutokana na mapigano hiuvi karibuni.

Taarifa ya Ofisi hiyo imesema wakati huu ambao jamii ya kimataifa inafuatilia uwajibishwaji kwa ajili ya ukatili dhidi ya raia katika kipindi cha miaka iliyopita, wanajeshi wa Myanmar wanatekeleza mashambulizi dhidi ya raia wake, mashambulizi ambayo yanaweza kuwa ukiukaji ambao unaweza kuwa ni uhalifu wa kivita na matokeo yake yanaweza kusababisha maafa.