Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani shambulio dhidi ya ofisi za UN Mogadishu

Mfanyakazi akiweka kibao kwenye ofisi  mpya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa ya usaidizi nchini Somalia, UNSOM mjini Mogadishu.
UNSOM
Mfanyakazi akiweka kibao kwenye ofisi mpya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa ya usaidizi nchini Somalia, UNSOM mjini Mogadishu.

Guterres alaani shambulio dhidi ya ofisi za UN Mogadishu

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio dhidi ya jengo la umoja huo kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

 Vyombo vya habari vinasema kuwa shambulio hilo la siku ya jumanne linafuatia kutua kwa makombora saba ndani ya jengo hilo ambapo watu watatu walijeruhiwa wakiwemo watumishi wawili wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo majeraha yao si makubwa sana kiasi cha kutishia uhai wao.

Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake amewatakia ahueani ya haraka majeruhi hao huu akisema kuwa shambulio lolote la makusudi dhidi ya watumishi wa Umoja wa Mataifa linaweza kuwa kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Amesihi mamlaka za Somalia zichunguze haraka shambulio hilo na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa vitendo vyaka hivyo hata hivyo havitofifisha azma ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kusaidia watu na serikali ya Somalia katika jitihada zao za kujenga amani, na utulivu nchini mwao.

Awali mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Haysom alitoa taarifa yake kulaani shambulio hilo ambalo tayari kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kimekiri kuhusika nalo.

Bwana Haysom amesema hakuna ajenda yoyote ya kisiasa ambayo inaweza kushughulikiwa kupitia ghasia ambazo moja kwa moja zinalenga watumishi wa mashirika ya kimataifa ambao wanasaidia mchakato wa kuimarisha amani na taasisi za kiserikali nchini Somalia.