Guterres amwondoa Haysom, kuteua mwakilishi wake mpya kwa Somalia

Nicholas Haysom, wakati akiwa Somalia akitekeleza jukumu lake la uwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa UN. Hapa akikutana na maafisa wa serikali ya Somalia mwezi Novemab mwaka 2018.
UNSOM
Nicholas Haysom, wakati akiwa Somalia akitekeleza jukumu lake la uwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa UN. Hapa akikutana na maafisa wa serikali ya Somalia mwezi Novemab mwaka 2018.

Guterres amwondoa Haysom, kuteua mwakilishi wake mpya kwa Somalia

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake kufuatia hatua ya serikali ya Somalia ya kumtangaza kutotakiwa na hivyo kutakiwa kuondoka nchini humo, mwakilishi wake maalum Nicholas Haysom.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres amesema ingawa kanuni hiyo ya kumtaka mwanadiplomasia kuondoka kwenye nchi au kutotakiwa kwenye nchi, kwa kilatini persona non grata, haitumiki kwa watendaji wa Umoja wa Mataifa kwa kuwa chombo hicho si nchi ameona ni vyema kumuondoa Bwana Haysom kwenye wadhifa huo ili Umoja wa Mataifa uweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha na kusaidia taifa hilo kupitia ofisi yake, UNSOM.

Kwa mantiki hiyo Guterres amesema ana nia ya kuteua mwakilishi mwingine ambaye pia atakuwa mkuu wa UNSOM, akisema ameazimia kuhakikisha mahitaji ya wananchi wa Somalia yanapatiwa kipaumbele kwenye kazi za Umoja wa Mataifa nchini humo na kuona chombo hicho kinaendelea kusaidia Somalia katika jitihada zake za kusaka amani, utulivu na ustawi kwa wote.

Katibu Mkuu amesema ana imani na Bwana Haysom, mtumishi wa umma wa kimataifa mwenye  uzoefu na anayeheshimika na ambaye ameweza kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi mashinani na kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kanuni ya persona non grata kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa 1961 Vienna kuhusu  uhusiano wa kidiplomasia inahusisha maafisa wa kibalozi au mawakala ambao wanawakilisha taifa kwa minajili ya uhusiano kati ya nchi mbili.

Watendaji wa Umoja wa Mataifa wanapofanya kazi katika nchi hawawakilishi taifa bali wanafanya kazi chini ya Katibu Mkuu.

Nicholas Haysom,(kulia) wakati alipowasili mjini Somalia mwezi Novemba mwaka 2018 akiwa na maafisa wenzake waandamizi wa UN
UNSOM
Nicholas Haysom,(kulia) wakati alipowasili mjini Somalia mwezi Novemba mwaka 2018 akiwa na maafisa wenzake waandamizi wa UN

Vyombo vya habari vilivyoripoti

Hivi karibuni vyombo vya  habari vilinukuliwa vikisema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilimwandikia barua Bwana Haysom ambaye ameshika wadhifa huo tangu mwezi Septemba mwaka jana, kuondoka nchini humo kwa madai ya kuingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.

Vyombo hivyo vilidai kuwa masuala hayo ni kitendo cha Bwana Haysom kuandika barua kuhoji hatua ya kiongozi wa zamani wa Al Shabaab Mukhtar Robow Abu Mansur kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa rais wa jimbo la Kusini-Magharibi nchini Somalia.

Wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi kuhusu Somalia, mwakilishi wa kudumu wa taifa hilo kwenye Umoja wa Mataifa alisihi kuheshimiwa kwa mamlaka ya taifa hilo lililopo pembe ya Afrika.

Guterres azungumza na Farmajo

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema, “katika siku chache zilizopita, Katibu Mkuu amezungumza mara mbili na Rais Mohamed Abdullahi "Farmajo" wa  Somalia. Tunasisitiza kuwa kanuni ya persona non grata haihusiki na wakati huo huo, ni muhimu kuwa ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Somalia uwe na uwezo wa kuendelea na kazi zake.”