Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 1 walifurushwa makwao DRC mwaka 2018

Wakimbizi waliotoroka vita nchini DRC wakiwa kwenye foleni wakisubiri kusajiliwa  na kuhakikiwa kwenye kituo cha uandikishaji cha Oruchinga nchini Uganda
Picha na UNHCR/Michele Sibiloni
Wakimbizi waliotoroka vita nchini DRC wakiwa kwenye foleni wakisubiri kusajiliwa na kuhakikiwa kwenye kituo cha uandikishaji cha Oruchinga nchini Uganda

Zaidi ya watu milioni 1 walifurushwa makwao DRC mwaka 2018

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu milioni moja wamefurushwa makwao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwa mwaka 2018 pekee kufuatia mzozo unaondelea nchini humo. Miongoni mwao ni Valentin Muhindo ambaye simulizi yake inaletwa kwako na Grace Kaneiya.

 

Katikati ya vilima kwenye eneo la Masisi, jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ni makazi ya mapya ya raia waliofurushwa makwao kutoka na mzozo mashariki mwa nchi.

Valentin Muhindo mwenye umri wa miaka 52 akiwa nje na familia yake, anasema alikimbia kijiji chao kidogo jimbo la Kivu Kaskazini mnamo Agosti mwaka 2018, wakati kundi la waasi waliojihami lilipowavamia.

(Sauti ya Valentin Muhindo)

“Tulishuhudia ukatili mwingi, tumeona watu wakiuawa, waasi walianza kuingia kwenye nyumba na kupora mali na mifugo, kuwapiga watu na tuliogopa. Tulikimbia bila chochote.”

Kwa sasa Bwana Muhindo anaishi katika eneo la Masisi ambako anafanya kazi ya useremala, akitumia vifaa vichache ambavyo alivibeba alipokimbia. Lakini hakuna kazi na anahaha kukidhi mahitaji ya wanae.

(Sauti ya Valentin Muhindo)

“Nina watoto wanane wangu na ninaishi na wengine wane ambao tulikutana nao njiani. Niliwahifadhi wakati tulikimbia kwa sababu walitenganishwa na wazazi wao.”

Ingawa vita vya wenyewe kwa wenyewe vimemalizika DRC, bado nchi hiyo imeendelea kukumbwa na visa vya mapigano hususan katika maeneo ya Mashariki mwa nchi.

Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa,  UNHCR mzozo unaoendelea unahatarisha watu wengi zaidi, Andreas Kirchhof ni Afisa wa masuala ya nje wa shirika hilo.

“Kuna makumi ya maelfu ya watu ambao wanaishi hapa kambini bila mwelekeo wowote na ambao wanataka kuanza maisha ya kawaida. Kwa sasa UNHCR inafanya kila iwezalo kusaidia wale wanaorejea nyumbani waweze kujumuika na familia na kusaidia wale ambao hawawezi kurejea kwa sasa kutokana  na sababu za kiusalama."

UNHCR imetoa wito kwa pande husika nchini DRC kuacha kulenga raia na wakati huohuo imeomba serikali itatue sababu za  watu kufurushwa na pia itafute suluhu kwa ajili ya waathirika.