Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia ihakikishe hakuna anayeachwa nyuma: UNCTAD

Kicheko kwa mtoto  huyu mkimbizi wa Syria huko Jordan akifurahia kujifunza kwa njia ya teknolojia mpya kwa kutumia lugha ya mama.
UNICEF/Herwig
Kicheko kwa mtoto huyu mkimbizi wa Syria huko Jordan akifurahia kujifunza kwa njia ya teknolojia mpya kwa kutumia lugha ya mama.

Teknolojia ihakikishe hakuna anayeachwa nyuma: UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Matokeo ya maendeleo ya teknolojia hayatabiriki lakini ni jukumu la kila mmoja, watunga sera katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia kuhakikisha kwamba dunia mpya ya kidijitali inaleta maendeleo kwa wote na hakuna anayeachwa nyuma. 

Hayo ni kwa mujibu wa Isabelle Durant, naibu katibu mkuu wa UNCTAD, akizungumza katika wiki hii ya biashara mtandaoni mjini Geneva Uswis, akisema kwamba anashawishika kuwa biashara ya mtandao na uchumi wa kidijitali vinatoa fursa kubwa.

Kuanzia uwezekano wa faida kwa makampuni ya nchi zinazoendelea katika nyanja mbalimbali ikiwemo gharama na bei nafuu, lakini pia vina uwezo wa kuwachagiza wanawake wajasiriamali.

UNCTAD inasema biashara ya mtandao au E-commerce ina uwezo wa kuwa muhimili wa mustakhbali wa mamilioni ya vijana barani Afrika na Amerika ya Kusini na uzuri wa ulimwengu wa kidijitali ni kwamba unaweza kuwaunganisha wafanyabiashara na masoko, lakini pia kuwaunganisha watu na huduma, hali ambayo itawasaidia sana hasa watu ambao wako katika maeneo yaliyojitengwa ambako huduma bado inaonekana kama kitu cha kifahari.

Hata hivyo pamoja na uzuri wake mafanikio haya sio kitu cha moja kwa moja, na ulimwengu wa kidijitali una changamoto zake na kama hakutakuwa na hatua nzuri zilizochukuliwa nasi unaweza kuongeza pengo baina ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea.

Na katika kuhakikisha ajenda ya maendeleo endelevu inatimia basi kila mmoja na kila mahali lazima ajumuishwe.