Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi wa utaifa wapunguza idadi ya wafanyakazi wanawake wahamiaji

Wafanyakazi wahamiaji wakiwa kazini katika kiwanda cha matofali huko Mawlamyine, Myanmar.
IOM
Wafanyakazi wahamiaji wakiwa kazini katika kiwanda cha matofali huko Mawlamyine, Myanmar.

Ubaguzi wa utaifa wapunguza idadi ya wafanyakazi wanawake wahamiaji

Wanawake

Shirika la kazi duniani ILO kupitia ripoti yake iliyotolewa leo  mjini Geneva Uswisi, linakadiria kuwa watu milioni 164 ni wafanyakazi wahamiaji , idadi hiyo ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia tisa tangu mwaka 2013 wakati idadi ilipokuwa watu milioni 150.

Kwa mujibu wa toleo la pili la makadirio ya kidunia kuhusu wafanyakazi wahamiaji wa kimataifa, makadirio ambayo yanaangazia kati ya mwaka 2013 na 2017, wengi wa wafanyakazi wahamiaji yaani milioni 96 ni wanaume, ilihali milioni 68 ni wanawake. Takwimu hizi zinaonesha kuwa kuna ongezeko la wafanyakazi wahamiaji wanaume kutoka asilimia 56 hadi asilimia 58, lakini upande wa wanawake asilimia zimepungua kiasi kwa pointi mbili kutoka asilimia 44 hadi 42.

Manuela Tomei, mkurugenzi wa idara ya hali ya kazi na usawa kwenye shirika la kazi duniani anasema, “pamoja na kuwa katika kipindi cha miongo miwili kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanawake ambao wamekuwa wakihama kwenda kutafuta ajira, ubaguzi ambao wanakutana nao kwa sababu tu ya jinsia yao na utaifa, vinapunguza fursa zao za ajira katika nchi wanamofikia ikilinganishwa na wenzao wa kiume.”

Ripoti hii inaendelea kueleza kuwa takribani aslimia 87 ya wafanyakazi wahamiaji wako katika umri wa kati wa ufanyaji kazi kwa maana kuwa tayari wana uzoefu, wengi wao wakiwa na umri kati ya miaka 25 na 64. Hii inamaanisha kuwa nchi kadhaa ambako ndiko watu hawa wanakotoka, zinapoteza sehemu muhimu ya nguvu kazi jambo ambalo linaweza kuwa na athari hasi katika ukuaji wa uchumi wa nchi hizo.

Ripoti imeonesha kuwa kati ya hao wafanyakazi wahamiaaji 164 duniani kote, takribani wafanyakazi milioni 111.2 yaani asilimia 67.9 wanaishi katika nchi zenye kipato cha juu, milioni 30.5 yaani asilimia 18.6 katika nchi za kipato cha kati, 16.6 milioni sawa na asilimia 10.1 katika nchi za kipato cha chini kati na wafanyakazi milioni 5.6 sawa na asilimia 3.4 wako katika nchi za kipato kidogo.