Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake katika uongozi huleta utendaji bora wa biashara.

Winnie Kakunta, msimamizi wa uendelezaji wa kampuni ndogo za kati katika Idara ya uhusiano wa jamii ya kampuni ya madini ya Barrick. Kampuni hii imeshirikiana na idara ya ajira bora nchini Zambia kujenga makazi kwa ajili ya wakazi na wafanyakazi wake.
ILO/Crozet M.
Winnie Kakunta, msimamizi wa uendelezaji wa kampuni ndogo za kati katika Idara ya uhusiano wa jamii ya kampuni ya madini ya Barrick. Kampuni hii imeshirikiana na idara ya ajira bora nchini Zambia kujenga makazi kwa ajili ya wakazi na wafanyakazi wake.

Wanawake katika uongozi huleta utendaji bora wa biashara.

Wanawake

Ripoti mpya ya shirika la kazi duniani, ILO imeonesha kuwa kampuni za kibiashara zenye uongozi wa ngazi ya juu ulio na mchanganyiko mzuri wa jinsia ya wanawake na wanaume zinapata faida kubwa. 

Ikiwa imetolewa leo huko Geneva, Uswisi ripoti hiyo yenye jina Wanawake katika biashara na usimamizi: Biashara kwa ajili ya mabadiliko, inatokana na utafiti wa takribani kampuni 13,000 katika nchi 70.

Zaidi ya asilimia 57 ya washiriki wa utafiti huu walikubali kuwa uwepo wa jinsia tofauti uliboresha matokeo ya biashara ambapo takribani robo tatu ya kampuni zenye mchanganyiko wa viongozi ziliripoti ongezeko faida kati ya asilimia 5 hadi 20, wengi wao wakishuhudia ongezeko kati ya asilimia 10 na 15.

Takribani asilimia 57 walisema ilikuwa rahisi kuvutia na kutunza vipaji huku zaidi ya asilimia 54 walisema waliona maboresho katika ubunifu, uvumbuzi na uwazi na pia idadi hiyo ilieleza kuwa ufanisi wa uwiano wa kijinsia uliimarisha sifa za kampuni zao.

Vilevile ripoti imegundua kuwa, katika ngazi ya kitaifa, ongezeko la ajira kwa wanawake lina uhusiano chanya na ukuaji wa pato la mwaka yaani GDP.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo, Deborah France-Massin, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya ajira ya ILO amesema makampuni kuwa na wanaume wengi kunawabana wanawake kupenya, kwa kuwa "kunavyokuwa na utamaduni zaidi wa kiume katika kampuni, kama naweza kuiweka hivyo, ndivyo kunakuwa na uwezekano mdogo wa wanawake kuweza kupanda hadi ngazi za juu. Na hiyo inaweza kuwa kwasababu kadhaa lakini bila kutaka tu mtu unajikuta unajisikia vizuri kufanya kazi na watu wa namna yako.”

Pia akaongeza sababu ya kihistoria, akisema kwamba “ninafikiri pia elimu ya wanawake ambapo, katika siku za nyuma, na hata sasa bado ni wanawake wachache wanaenda katika masomo ya sayansi na teknolojia, pia wanawake wachache wanachukua masuala ya uchumi au uzalishaji bidhaa”

Aidha Bi. Massin ameongeza katika zama za uhaba wa ujuzi, wanawake wanawakilisha vipaji lukuki ambavyo makampuni hayajatumia.”

Hata hivyo ripoti imetaja kuwa baadhi ya sababu zilizotajwa kuwafanya wanawake kutofikia ngazi za juu za maamuzi ni utamaduni wa kampuni wa ‘popote, muda wowote’ ambao unawaathiri wanawake kutokana na majukumu yao ya kifamilia.

Uwiano wa kijinsia katika uongozi wa ngazi za juu unatafsiriwa kuwa ni asilimia 40 kwa 60 wa jinsia yoyote.

Ripoti inasema faida ya mchanganyiko wa kijinsia inaanza kuonekana pale ambapo wanawake wanashikilia asilimia 30 ya ngazi za juu za uongozi. Hata hivyo takribani asilimia 60 ya makampuni hayafikii lengo hili.