Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchumi wa dunia wadorora, chonde chonde watunga sera msipeleke chombo mrama- IMF

Makao makuu ya shirika la fedha duniani la IMF la mjini Washington, DC Marekani
Picha ya IMF/Henrik Gschwindt de Gyor
Makao makuu ya shirika la fedha duniani la IMF la mjini Washington, DC Marekani

Uchumi wa dunia wadorora, chonde chonde watunga sera msipeleke chombo mrama- IMF

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la fedha duniani, IMF limesema uchumi wa dunia unasuasua na hivyo linataka viongozi duniani wawe makini katika kile wanachofanya.

Mchumi mkuu wa IFM Gita Gopinath amesema hayo leo mjini Washington, DC nchini Marekani wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwelekeo wa uchumi duniani.

Gopinath, ambaye ni mwanamke wa kwanza kushikwa wadhifa huo kwenye IMF amewaambia waandishi wa habari kuwa, “uchumi wa dunia unazidi kudhoofika na kusinyaa. Asilimia 70 ya uchumi wa dunia unatarajiwa kudhoofika kwa mwaka huu wa 2019 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Tunatarajia ukuaji mwaka 2020 ingawa bado tunaona kuna hatari kubwa.”

Amesema sababu kuu ya kudorora kwa uchumi ni mivutano ya kibiashara na mazingira magumu ya kifedha mwishoni mwa mwaka 2018 akiongeza kuwa, “hatari kubwa inaendelea kwenye mvutano wa kibiashara. Hivi sasa tumeona kuna maendeleo kwenye mazungumzo ya kibiashara kati ya China na Marekani. Hata hivyo tuna wasiwasi kuwa mvutano wa biashara unaweza kuongezeka na inaweza kudhihirika kwenye sekta nyingine kama vile ya magari ambazo zinaweza kuharibu uchumi wa dunia.”

Mchumi mkuu huyo wa IFM amesema wakati kasi ya ukuaji inadorora, kuna njia ambazo kwazo watunga sera wanaweza kuhamasisha ukuaji kwa muda wa kati na kupunguza hatari za kudorora kabisa kwa uchumi.

Akifafanua Gopinath amesema “ni hali tete hivi sasa kwa uchumi wa dunia. Ni muhimu sana kwa watunga sera wasichukue hatua za kufanya hali kuwa mbaya zaidi na badala yake washirikiane kupunguza kiwango cha juu cha ukosefu wa uhakika wa mwelekeo wa uchumi duniani hususan suala la sera za biashara.”

Halikadhalika amesema ni muhimu kwa mbinu makini za uchumi mkuu zikatumika ili kuhakikisha hatari za kifedha hazinyemelei kudororesha uchumi zaidi, na sera za fedha zinasimamiwa vyema kupunguza mvutano kati ya hamu ya ukuaji wa uchumi na usimamizi thabiti wa deni ili liwe endelevu.