Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umaskini watishia hali ya misitu ukanda wa Mediteranea- Ripoti

Misitu bora na endelevu ni makazi bora ya nyuki
UNMISS/Eric Kanalstein
Misitu bora na endelevu ni makazi bora ya nyuki

Umaskini watishia hali ya misitu ukanda wa Mediteranea- Ripoti

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya ya mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa na wadau wake kuhusu hali ya misitu kwenye ukanda wa Mediteranea inaonyesha kuwa maliasili hiyo iko kwenye tishio kubwa licha  ya umuhimu wake kwa viumbe ya nchi kavu na baharini.

Ikiwa imeandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo, FAO, mazingira, UNEP na wadau wake MAP na Plan Bleu, ripoti inasema tishio kubwa katika ukanda huo unaojumuisha nchi 31 linatokana na mabadiliko ya tabianchi, umaskini, na ongezeko la idadi ya watu.

“Bila ya kupatia kipaumbele malengo mawili maendeleo SDGs, ukanda huo utakuwa hatarini zaidi,” imesema ripoti iyo ikitaja malengo hayo kuwa ni lile namba 15 la kulinda, kuhifadhi na matumizi endelevu ya bayonuai na lengo namba 6 la matumizi endelevu ya maji na huduma za kujisafi.

Hata hivyo tayari ripoti imetaja baadhi ya hatua ambazo zinachukuliwa ili kukabiliana na matumizi endelevu ya misitu ikiwemo miradi mbadala kwa wakazi wanaotegemea misitu kwa ajili ya nishati, kujipatia kipato, malisho ya wanyama na shughuli za kilimo.

“Mipango na miradi kuzunguka eneo la Mediteranea tayari inachangia katika kupunguza umaskini na kufanikisha lengo namba moja la SDG la kuondoa umaskini. Nchini Tunisia kwa mfano, mashirika ya kijamii na sekta binafsi wanashirikiana katika usimamizi wa misitu na kutumia vizuri maeneo ya ardhi pamoja na misitu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa FAO idara ya misitu, Hiroto Mitsugi na akichangia katika utangulizi wa ripoti hiyo amesema, “bidhaa na huduma kutoka misitu ya ukanda huo wa Mediteranea ni rasilimali muhimu ambazo kwazo ni vyema juhudi kufanyika kuilinda.”

Amesema uhifadhi wa misitu, ardhi na mipango bora ya kutumia misitu hiyo na kulinda bayonuai ni hatua bora za kusaidia eneo hilo kuhifadhiwa kwa maslahi ya wakazi awke na mazingira.

Eneo la misitu la  ukanda wa Mediteranea lina  ukubwa wa zaidi ya heka milioni 25 za misitu ambazo ni chanzo cha mbao, chakula, nishati, dawa, maji na fursa zingine kama kurina asali, utalii na ajira.