UN-REDD yasaidia mataifa kusimamia vyema misitu

19 Oktoba 2018

Programu ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia nchi wanachama kupunguza utoaji wa hewa chafuzi utokanao na ukataji hovyo misitu imekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu imeziwezesha kufuatilia misitu yao ipasavyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO ambalo kwa kushirikiana na shirika la mazingira duniani, UNEP ndi wanasimamia mradi huo uliopatiwa jina UN-REDD, kule ambako mradi umetekelezwa serikali  zimeweza kuboresha mifumo yao ya kitaifa ya kufuatilia misitu na hivyo kuwa na takwimu sahihi pamoja na ramani za maeneo yenye misitu ambayo awali ilikuwa ngumu kuzipata.

Mathalani, mfumo huo wa ufuatiliaji wa misitu umewezesha serikali 34 kuwasililisha kwenye sekretarieti ya mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC takwimu zinazoonyesha kiwango cha hewa ya ukaa inayofyonzwa na misitu ambayo nchi hizo zinahifadhi.

“Nchi hizo 34 kwa ujumla zina jumla ya eka bilioni 1.4 za misitu ambayo ni sawa na asilimia 36 ya eneo la misitu yote duniani,” imesema taarifa hiyo ikieleza kuwa “takwimu hizo ni msingi muhimu kwa mataifa hayo kuweza kulipwa fedha za fungu la biashara ya hewa ya ukaa.”

Mradi huo wa UN-REDD ulianzishwa kwa pamoja na FAO na shirika la mazingira duniani, UNEP mwaka 2008 ili kusaidia nchi zinazotaka kushiriki kwenye biashara hiyo ya hewa ya ukaa.

Biashara ya hewa ya ukaa inahusisha malipo kwa mataifa ambayo yanahifadih eneo la misitu itakayofyonza hewa ya ukaa inayozalishwa na mataifa mengine kwa lengo la kupunguza kiwango cha hewa chafuzi zinazotoboa tabaka la ozoni.

Pamoja na kupata malipo hayo, nchi zilizoshiriki UN-REDD zimewezeshwa kutunga mikakati ya kitaifa ya ufuatiliaji misitu kwa kuzingatia kuwa vitendo kama vile upanuzi wa mashamba, ubadilishaji maeneo ya mashamba kuwa malisho pamoja na ukataji wa magogo na uchomaji moto misitu huchangia asilimia 11 ya hewa chafuzi duniani.

Akizungumzia ripoti hiyo, mratibu wa REDD katika FAO Tiina Vahanen amesema kuwa na misitu ambayo ina uwezo wa kufyonza kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa, ni mfumo bora zaidi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo amesema “ili kuweza kutumia vyema mfumo huu tunahitaji mifumo thabiti, ya kuaminina kuhusu kile kinachoendelea kwenye misitu.”

Ripoti ihyo ya tathmini imezinduliwa katika kikao ha bodi tendaij ya UN-REDD huko Roma, Italia ambapo nchi zilizohusika kwenye tathmini hiyo ni 16 kati ya 64 ambazo zinatekeleza UN-REDD nazo ni Cambodia, Colombia, Côte d'Ivoire, DR Congo, , Ecuador, Indonesia, Laos, Nigeria, Panama, Papua New Guinea, Paraguay, Sri Lanka, Tanzania, Viet Nam na Zambia.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter