Hatua shirikishi ni muarobaini wa kulinda misitu- FAO

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya misitu duniani imezitaka serikali kuchukua hatua jumuishi katika ulinzi na uhifadhi wa misitu ili kupunguza kasi ya kupungua kwa eneo la misitu kila uchao.
Kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO ambalo ndio mwandishi wa ripoti hiyo, hatua kama vile kupunguza ukataji miti holela, matumizi endelevu ya misitu na kupanda miti ni hatua ambazo zinapaswa kutekelezwa kwa kutumia jamii zinazonufaika na rasilimali za misitu.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva amesema hatua hizo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa misitu ni rasilimali adhimu kwa vipato na uhai wa binadamu, akisema misitu bora ni muhimu kwa kilimo endelevu na maji bora.
Kwa mantiki hiyo ripoti inasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo ya uwazi ya haki za kumiliki misitu na inapongeza mwenendo wa sasa wa serikali za mitaa kushirikishwa katika usimamizi,bila kusahau ubia wa sekta binafsi na ile ya umma.
Nchini Tanzania tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kulinda misitu ikiwemo kushirikisha jamii kama anavyoeleza Dkt. Ezekiel Mwakalukwa, Mkurugenzi wa Idara ya misitu na Nyuki kwenye wizara ya maliasili na utalii ya nchi hiyo.
(Sauti ya Dkt. Ezekiel Mwakalukwa)
Hata hivyo ripoti inasema ingawa bado kuna kazi kubwa ya kufanya, tayari kuna maendeleo ikitolea mfano ongezeko la uelewa katika matumizi endelevu ya misitu.
Mathalani zaidi ya asilimia 56 ya karatasi zinazotumika hivi sasa ni zile zilizohuishwa ikiwa ni ongezeko kutoka chini ya asilimia 25 mwaka 1976.
Mafanikio mengine ni utengenezaji wa paneli za mbao kwa kutumia mabaki ya taka hali ambayo imepunguza matumizi ya miti kwenye kutengeneza samani.
Ripoti hii mpya imeandaliwa kuelekea jukwaa la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu litakalofanyika jijini New York, Marekani tarehe 9 mwezi huu.